MATUMIZI ya dawa za kulevya, yanatajwa na wataalamu wa afya ya ubongo na uti wa mgongo kuwa ni kisababishi cha msongo wa mawazo na magonjwa ya akili.
Kwa mujibu wa wataalamu hao, kutumia dawa hizo, kunaathiri zaidi sehemu za ubongo zilizo karibu na sikio, na kwamba hapo kuna sehemu ya ndani zaidi inayohusika na kazi mbalimbali kama kuhifadhi kumbukumbu za muda mfupi za matukio mbalimbali.
Wabobezi wa afya wanafafanua kuwa, sehemu hiyo pia inafanya kazi ya utambuzi wa hisia ikiwamo furaha au huzuni na kwamba kutumia dawa kunaingilia mfumo huo na kusababisha ushindwe kufanya kazi kwa namna inavyotakiwa.
Inaelezwa kuwa, kutumia dawa hizo kunapokithiri na mtumiaji anapofikia katika hali hiyo, mwathirika anaweza kujikuta anakumbana na tatizo la afya ya akili na kwamba, madhara ya dawa hizo ndiyo yanayosababisha zipigwe marufuku duniani kote.
Maelezo hayo ya wataalamu wa afya, yanaonyesha wazi kwamba kuna umuhimu wa kuwa makini au kuwaelimisha na kuwalinda vijana ili waepuke kuingia katika matumizi ya dawa hizo hatari kwa afya. Ripoti ya Dunia ya Dawa za Kulevya mwaka 2023 iliyozinduliwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), inaonyesha kuwa zaidi ya watu milioni 296 duniani wanatumia dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, vijana ndio walio hatarini zaidi kutumia dawa za kulevya na kuathirika zaidi na ugonjwa wa matumizi ya dawa hizo duniani huku Afrika ikiwa na asilimia 70 ya watu wanaopata matibabu dhidi ya dawa hizo wengi wakiwa chini ya umri wa miaka 35.
Kwa Tanzania, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) inaendelea kuwasaka wanaofanya biashara ya dawa hizo, katika maeneo mbalimbali ili kulinda afya za Watanzania. Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, anasema Aprili 4 mwaka huu, mamlaka hiyo ilikamata kilo 767.2 za dawa za kulevya katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga.
Lyimo katika ufafanuzi wake, anataja aina ya dawa zilizokamatwa zilikuwa ni pamoja na heroine kilo 233.2, methamphetamine au ‘metha’ kilo 525.67 na skanka kilo 8.33, huku watu 21 nao wakikamatwa. Wakati huu ambao mamlaka hiyo inaendelea na msako, inatoa tahadhari kwa madereva wa mabasi na makondakta kuwa wawe makini, kwa kuwa mabasi hayo yamekuwa yakitumika kusafirisha dawa hizo.
Mamlaka hiyo inasema imebaini kuwa, kwa sasa mabasi yanatumika kama njia ya kurahisisha usafirishaji wa dawa hizo kwenda maeneo mbalimbali nchini na kwamba madereva na makondakta wawe makini. "Ninawatadharisha madereva wa mabasi kwamba wawe makini, tukikuta basi linasafirisha dawa hizo, tutawakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria," ndivyo anavyosema Kamanda Lyimo.
Huo unaweza kuwa mtihani kwao, kwa sababu sio wataalamu wa kutambua dawa hizo, ninadhani ni vyema mamlaka hiyo ikawapa elimu ili iwe rahisi kutambua dawa hizo na kutoa taarifa. Kwa nini? Kwa sasa mamlaka hiyo inasema imebaini mbinu mpya ya ufichaji wa dawa za kulevya inayotumiwa kuzificha kwa ustadi katika vifungashio vilivyoandikwa majina ya kahawa au chai.
Hivyo, kwa mbinu hizo, madereva na makondakta wanaweza kujikuta katika mtihani mkubwa iwapo DCEA itaamua kukomaa nao katika ukaguzi wa dawa hizo katika mabasi.
Kwa mbinu hiyo ya DCEA, makondakta na madereva wawahusishe wataalamu wa dawa za kulevya kupima vifurushi hivyo kabla ya kukabidhiwa kwao ili kuvisafirisha.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED