CHAMA cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kinafanya uchaguzi wake wa kupata viongozi katika nafasi mbalimbali mwaka huu ikiwamo ya urais na makamu wake.
Kinachoibua maswali kwenye mchakato huo ni suala la wanawake kutojitokeza katika kinyang`anyiro cha urais.
Chama hicho chenye miaka 70, kiliundwa wakati wa ukoloni wa Uingereza 1954, kimeongozwa na wanawake wawili pekee Jaji Joaquine De Mello na Fatuma Karume.
Ushiriki wa wanawake ni muhimu kwa sababu hata katika michezo ya dunia ya Olympiki inayoendelea Ufaransa usawa wa kijinsia umezingatiwa ukiwa na uwakilishi wa 50/50.
Aidha, kwenye kinyang`anyiro hicho cha urais, wagombea katika uchaguzi huo mwaka huu, wako wanaume sita bila mwanamke, licha ya kwamba yuko mmoja anayegombea nafasi ya makamu wa rais.
Jumamosi iliyoisha, kulikuwa na mdahalo wa wagombea hao sita wa nafasi ya urais ulioendeshwa na moja ya kituo cha runinga ukirushwa mubashara ambapo kila mmoja alielezea mipango mikakati yake (sera) kwa watazamaji walioshiriki mdahalo huo, aidha watu wanahoji sababu za kukosekana sura ya mwanamke kugombea nafasi hiyo.
Moja ya jibu wanalopewa ni kwamba huenda wanawake wanaogopa kujitokeza katika nafasi hiyo kutokana na hali ya ushindani wa nafasi yenyewe kwa sasa.
Kwamba, kwa sasa kushindania nafasi ya urais TLS inahitaji kutumia ‘misuli’ hivyo wanawake wengi wanaogopa na ndiyo maana wanaamua kujitokeza kwenye nafasi za chini kidogo.
Kinachoibuka TLS leo kiwaamshe wanaharakati wanaotetea haki za wanawake wakiwamo wanasheria wanawake walioko Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA), Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake(WLAC) na vingine kama hivyo vijitokeze kuwapendekeza wanawake wa kuwania nafasi hizo na kuwaunga mkono.
Ni vema wanasheria wanawake watumie vyama vyao kutoa nafasi na ushiriki kwa wanawake wa kuwawakilisha kugombea nafasi hizo na kuwa mstari wa mbele kuwaunga mkono bila kujali itikadi na mitizamo.
Tunatambua kwamba hulka ya mwanamke si kutumia nguvu au mabavu zaidi katika kupata kitu kama ilivyo kwa mwanamume na kama inavyoonekana kwamba kwa mwanamke mmoja kujitosa peke yake katikati ya kundi la wanaume kuwania nafasi ambazo wakati mwingine zinaambatana na kampeni ngumu.
Kuna haja kwa vyama hivyo vya wanasheria vya wanawake, vinaunganishe nguvu ya pamoja kumpigia kampeni mwenzao anayeaminika kuwa na uwezo wa kukiongoza chama.
Pia, serikali inahitaji kuonesha dhamira ya kisiasa kuwekeza kwenye usawa wa kijinsi siyo TLS pekee bali kwenye maeneo mengine mfano kwenye ukuu wa taasisi za umma.
Kwa mfano, kuna mchakato wa kuboresha Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, ni vema nayo ikaweka mkazo kuhusu usawa wa jinsia katika nafasi za uongozi kwenye taasisi na asasi mbalimbali za umma na binafsi.
Kwa mfano chuo kikuu kikongwe cha Dar es Salaam, hakijawahi kuwa na Makamu Mkuu wa Chuo mwanamke. Kadhalika, Mwanasheria Mkuu wa serikali hajawahi kuwa mwanamke.
Ni wakati sasa umefika wa kuwa na Jaji Mkuu mwanamke ambaye tangu uhuru hadi sasa hakujawahi kutokea.
Ni vyema kuangalia upungufu unaojitokeza TLS leo na kujifunza kuwa hilo ni tatizo kubwa ambalo linahitaji kufanyiwa kazi ili kufikia ajenda ya uwakilishi wa 50/50.
Kadhalika, katiba na sheria ziweke wazi kuwa ni wakati wa kuwa na usawa wa kijinsia kwenye ngazi zote za uongozi na taasisi za kitaifa zinazowakilisha maoni shirikishi kama ilivyo TLS.
Bila kujali ni ukweli kuwa wanawake ndilo kundi kubwa la zaidi ya nusu ya raia wa nchi hii ambao ni zaidi ya milioni 61, inakuwaje waachwe kwenye mipango ya uongozi, uwakilishi na mipango ya maendeleo?
Baadhi ya wagombea hao wa nafasi ya urais TLS wameliona hilo na wakasikika wakisema endapo watachaguliwa watahakikisha wanaweka sera ambayo itawezesha usawa huo wa kijinsia, ni vema ikawa hivyo katika taasisi zote.
Uchaguzi wa TLS hufanyika kila mwaka japo kiongozi anaruhusiwa kugombea kwa vipindi vyote hivyo vitatu na akachaguliwa na mwaka huu unatarajiwa kufanyika kuanzia Jumatano hadi hadi Ijumaa wiki hii jijini Dodoma.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED