Tahadhari dhidi ya homa ya nyani

By Moshi Lusonzo , Nipashe
Published at 10:25 AM Aug 08 2024
Mgonjwa wa Mpox.
Picha: Mtandao
Mgonjwa wa Mpox.

KAMA mataifa jirani ikiwamo Kenya yamethibitisha kuwa na wagonjwa wa homa ya nyani maarufu kama monkey pox au ‘Mpox’ Tanzania, sisi ni nani tusichukue tahadhari?

 Katika taarifa inayotolewa na Wizara ya Afya ya Kenya, mgonjwa mmoja amegundulika Mombasa eneo linalopakana na Tanzania upande wa Kusini Mashariki.

Tayari ugonjwa huo umeripotiwa kusambaa kwa kasi  huko Congo (DRC), Rwanda, Burundi na Afrika ya Kati.

Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa tahadhari ya kuibuka kwa virusi vipya vya homa hiyo kali ambayo tayari imeua idadi kubwa ya watu nchini DRC.

Kutokana na ugonjwa huo kuenea kwa kasi kutoka taifa moja hadi lingine, serikali   ya Tanzania inatakiwa kutambua kuwa, ugonjwa huo umepiga hodi na kunahitajika jitihada za kuzuia kuingia nchini ili kuepusha kutokea kwa madhara yanayotokana na ugonjwa huo kama inavyotokea mataifa jirani.

Inaelezwa kuwa, ugonjwa huo unaambukizwa kwa kugusa majimaji kutoka kwa mtu anayeugua au kuambukizwa, hivyo ni rahisi kusambaa endapo watu hawatachukua tahadhari za kujilinda ikiwamo kunawa mikono.

Kama tayari Kenya na Uganda zimeripoti kuwapo kwa maambukizi hayo, hivyo ni rahisi kuingia nchini kutokana na mwingiliano baina ya Watanzania na watu nchi hizo. Hii inatokana na sababu mbalimbali hasa shughuli hasa za kiuchumi na kijamii.

Aidha, Wizara ya Afya ina wajibu wa kuwaelimisha watu jinsi ya kujilinda  na ugonjwa huo kwa kutumia njia mbalimbali ikiwamo vyombo vya habari, vipeperushi na kuweka matangazo mtaani.

Pamoja na serikali kueleza kuwa ipo makini na ugonjwa huo, lakini inatakiwa kufanya juhudi zaidi kwa kuwapeleka maofisa wa afya katika maeneo ya mipakani, vijijini na katika miji ya mipakani kuwapa elimu wananchi ambao hawana ufahamu wa maradhi hayo.

Homa ya nyani, ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vya nyani na dalili zake ni pamoja na kutokwa damu’

Licha ya ugonjwa huo kuenea kwa njia ya kama vile kugusana moja kwa moja na mtu iliyeambukizwa, majimaji ya mwili kama damu, jasho, mate na haja ndogo si kitu cha kupuuzwa.

Inaelezwa kuwa, unaweza kuambukizwa kupitia mate mtu anapokohoa hivyo tahadhari ni muhimu.

Dalili kubwa ni mtu kupata upele kwenye ngozi, vidonda mdomoni na sehemu za siri.

Hata hivyo, Mpox hutibika bila ya matatizo ndani ya wiki mbili hadi nne.

Pamoja na ugonjwa huo kuwa na tiba, serikali kupitia wizara mbalimbali  ingeendesha zoezi la kutoa chanjo kwa watu wanaoishi katika maeneo yanayotiliwa shaka hasa mipakani.

Kama tulivyovuka salama katika janga la UVIKO-19, baada ya elimu ya kutosha kutolewa pamoja na kutoa chanjo, ni wazi hata kwa ugonjwa huu serikali inaweza kupambana na hatimaye ukaishia nje ya mipaka yetu.

Pia, vitengwe vituo maalumu vya kutolea matibabu kama ilivyo kwa magonjwa mengine ya mlipuko, pamoja na kuujulisha umma mahali vilipo ili patakapotokea tatizo hilo iwe rahisi kukimbilia.

Mathalani, katika maeneo ya mipakani, viwanja vya ndege na vituo vya mabasi, kuwapo na vipimo vya kuangalia viwango vya joto kwa watu wanaotoka katika nchi zilizothibitisha kuwapo kwa ugonjwa huo nchini mwao.

Serikali iweke mkakati maalumu kwa kuwatambua watu wanaovuka mipaka kwa njia haramu, hivyo njia hii itafaulu kama watashirikishwa viongoizi wa serikali, kidini na kisiasa katika kuwaelemisha wananchi.

Kwa upande wa wananchi nao wanawajibu kufuata yale yanayoelezwa kutoka vyanzo muhimu vya afya, na tuache masuala ya kupuuzia kwani akipata mtu mmoja basi atayaweka hatarini maisha ya watu wengi.

Tuache tabia ya kuwahudumia watu wenye matatizo kabla ya kuwafikisha hospitali. Ukipata mgeni mwenye tatizo linaloambatana na dalili za homa ya nyani, ni muhimu kumuwahisha hospitali, badala ya kumpatia matibabu nyumbani.

Kwani kwa kufanya hivyo ni kuhatarisha maisha ya watu wengine na kuliingiza taifa kwenye janga kutokana na kupuuza maelekezo.

Tunaipongeza serikali kwa kutoa taarifa mapema kuhusu maendeleo ya ugonjwa huo katika nchi za jirani kwani hatua hiyo imewafanya watu kuwa na tahadhari.

Taarifa kama hizo ziendelee kupatikana kila mara ili kuwafanya watu kupata habari sahihi na kwa wakati kuhusu ugonjwa huo.

Kufaulu kuepukana na ugonjwa huu hatari kutatokana na ushirikiano kati ya serikali na wananchi. 

Waswahili wanasema ‘kinga ni bora kuko tiba’, hivyo wote tushikamane tujilinde dhidi ya ugonjwa huu badala ya kuhangaikia tiba ambayo ni gharama kwetu sote.