Siasa zetu zilenge R4 za Rais Samia

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 10:36 AM Aug 14 2024
Rais Samia Suluhu Hassan.
Picha: Ikulu
Rais Samia Suluhu Hassan.

MJADALA unaoendelea kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari wiki hii ni taarifa zilizopewa uzito kwenye magazeti ni kuhusu kusitishwa kwa maandamano ya CHADEMA, yaliyolenga kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani.

CHADEMA ilipanga kufanya maandamano na kisha mkutano wa hadhara katika uwanja wa Ruanda Nzovwe, jijini Mbeya, Jumatatu wiki hii  yaliyoshajihishwa na kauli za Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (BAVICHA), John Pambalu, aliyewataka vijana wajitokeze kwa wingi kuamua hatima ya taifa lao.

Kiongozi huyo akiwataka vijana wawaige wenzao wa Kenya, ambao waliandamana kulishinikiza bunge lao lisipitishe sheria ya fedha ya mwaka 2024/25.

Baada ya kufuatilia vuta nikuvute baina ya chama hicho na polisi na madai ya viongozi wa juu wa chama hicho kushikiliwa kuanzia juzi, kuna mambo kadhaa yanayoibuka.

Mosi, Kenya waliandamana kwa hoja mahsusi ya kupinga muswada wa fedha, ambao uliwaunganisha na kuiwajibisha serikali yao. Kilichotokea Kenya baada ya Rais William Ruto, kukubaliana na waandamanaji hadi kuvunja baraza lake la mawaziri, ni fujo.

Kwa yeyote makini anayefuatilia siasa za majirani hao, atabaini kwamba waandamanaji wamefanya uharibifu usiopimika. Tuliofuatilia maandamano yale kuanzia hatua za awali, tuliona kijana akiwa amebeba siwa ya bunge la nchi hiyo  mtaani.

Kadhalika jengo la bunge hilo liliharibiwa, majengo ya umma na mali nyingi zikichomwa moto.

Baada ya kauli za baadhi ya viongozi wa CHADEMA, polisi ambayo ina wajibu wa kulinda usalama wa raia na mali zake, wakasimama kwenye nafasi yao kuzuia fujo ambazo bila shaka zingeweza kuitumbukiza nchi kwenye hasara kubwa.

Tumeshuhudia kwenye maandamano ya majirani, majeruhi na vifo vikiripotiwa huku mamia ya wananchi wakipoteza mali. Nafikiri, Tanzania tunapaswa kujifunza namna bora ya kuilinda nchi yetu isifike huko. Tufanye mjadala, tushindane kwa hoja bila fujo wala kuumizana; huku tukizingatia R4 za Rais Samia Suluhu Hassan, ambazo ni Maridhiano, Mabadiliko, Ustahamilivu na Kujenga Taifa Upya.

Siungi mkono chama chochote cha siasa kunyimwa kufanya mkutano, lakini sikubaliani kuwapo na vurugu za kisiasa. Nasema hivi kwa sababu, polisi walikuwa na sababu za kuzuia maandamano ili Tanzania isiwe kama Kenya ambayo hivi sasa imeshapata hasara kubwa kwa biashara na shughuli za uzalishaji za wananchi  kuumizwa kwa kiasi kikubwa.

Kitendo cha Jeshi la Polisi kuwaachia  huru wafuasi na viongozi wa CHADEMA ni kutimiza ustahamilivu

na R4  za Rais Samia. Ni kwa sababu, kama waliokamatwa wiki hii wangekamatwa kipindi cha awamu ya tano leo wangekuwa wamefunguliwa kesi za uchochezi na wangekuwa mahabusu wakisubiri kupelekwa mahakamani.

Bila shaka, wanaofuatilia utekelezaji wa R4  za Rais Samia, watakubali  kwamba hazimaanishi

kuruhusu fujo. Aidha si kwa ajili ya kufanya siasa zinazolenga kuleta machafuko kwenye taifa ambalo limekuwa mfano wa kuigwa wa amani na utulivu barani Afrika na duniani pia. 

Tukumbuke, Wakenya wameandamana kwa sababu waliyoiweka bayana kama kuikataa sheria

ya fedha. Sababu hii iliungwa mkono wazi wazi na asilimia kubwa zaidi ya wananchi wasiofungamana

na mirengo ya kisiasa, na zikakosa muafaka wa kitaifa. Tanzania hatujafika huko. 

Hoja nyingi zinatatuliwa kwa majadiliano kwenye msingi wa R4 na kilichofanywa na polisi kuwakamata baadhi ya viongozi ni kuepusha uvunjifu wa amani. Dhana ya R4  ya Rais Samia imetumika kuwaachia bila kuwaumiza wala kuwafungulia kesi.

Ninachoweza kusema ni kwamba  dhana  hiyo haina maana ya kuruhusu fujo au ‘uholela’ wa kisiasa bali kushirikiana kuijenga nchi na kuwa na Tanzania inayoimarika kiuchumi na  kidemokrasia.