Morogoro ongezeni kasi sekondari mkoa wenu

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 07:06 AM Aug 07 2024
Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda.
Picha: Mtandao
Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda.

SAYANSI ni moja ya masomo ambayo kwa muda mrefu yanakimbiwa na baadhi ya wanafunzi wasichana kutokana na dhana iliyojengeka miongoni mwao kuwa ni magumu hasa pale yanapohusisha na hesabu.

Ili kuondoa dhana hiyo, kuna jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali pamoja na wadau wa elimu, kuanzia kutoa motisha, kuongeza shule za sayansi na kuhamasisha wasichana kupenda masomo hayo na kuelezwa kuwa siyo magumu kama wanavyodhani.

Jitihada za hivi karibuni ni ujenzi wa shule za sekondari za wasichana za masomo ya sayansi kila mkoa, kupitia mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP).

Hatua hiyo, inalenga kuifanya idadi ya wanafunzi wa kike iwe sawa na wavulana katika masomo hayo ili hatimaye kuwe na wataalamu wengi wa kike wa fani mbalimbali kama walivyo wa kiume.

Hadi kufikia sasa, sekondari 25 zimeshajengwa katika mikoa 25 na zimeanza kupokea wanafunzi, huku mkoa mmoja ambao ni Morogoro, ukiendelea na kazi ya ukamilishaji wa sekondari hiyo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa ndiye aliyasema hayo hivi karibuni, akifafanua kuhusu hatua ambazo zimechukuliwa na serikali.

Katika ufafanuzi wake, anasema serikali ilishatoa Sh. bilioni 104 kati ya Sh. bilioni 106.6, zilizotengwa kwenye bajeti, kwa ajili ya ujenzi wa shule sekondari hizo ambayo ni sawa na asilimia 98.

Binafsi, ninaunga mkono juhudi zinazochukuliwa na serikali za kutaka kuhakikisha wasichana wanapata fursa ya kusoma masomo ya sayansi ambayo kwayo muda mrefu wamekuwa wakiyakwepa.

Hatua hiyo inayochukuliwa na serikali, inalenga kuwafanya wasichana wawe na ujuzi katika sayansi, teknolojia na ubunifu, hasa kwenye dunia hii ya sasa ambayo tunashuhudia mabadiliko mbalimbali ya kimaendeleo.

Hongera kwa mikoa 25 ambayo imekamilisha ujenzi wa sekondari hizo za wasichana na kuanza kuchukua wanafunzi, lakini Mkoa wa Morogoro uongeze kasi ili ukamilishe sekondari hiyo.

Matarajio ya serikali na wadau wa elimu, ni kuona nchi inapiga hatua  katika masomo ya sayansi, kwa wasichana ili walete ushindani kwa wenzao wa kiume ambao kwa muda mrefu wamekuwa mstari wa mbele.

Jitihada za ujenzi wa shule hizo ni kuleta usawa wa kijinsia kwa wasichana katika kusomea masomo ya sayansi ili baadaye wapewe fursa za ubunifu au maendeleo kama ilivyo kwa wanafunzi wa kiume.

Vilevile, hatua zilizochukuliwa na serikali za kujenga sekondari za wasichana za masomo ya sayansi, zinaonesha kuwa dhana ya kuwa masomo ya sayansi ni magumu kwa wasichana haina nafasi tena.

Hivyo, ukamilishaji wa sekondari hizo ni hatua muhimu kwa malengo ambayo serikali imejiwekea ya kuinua wasichana kupitia masomo ya sayansi, ndio maana nikashauri Mkoa wa Morogoro nao uharakishe kukamilisha sekondari ya mkoa kama ilivyo kwa mikoa mingine 25.

Nguvu kubwa kwa sasa imeelekezwa katika kuwahamasisha wasichana kusoma masomo ya sayansi ili kutengeneza usawa, kwa kuweka hamasa katika masomo hayo, ni vyema hilo lingezingatiwa na kila mkoa.

Mkoa wa Morogoro ongezeni kasi, ama jifunzeni mbinu zilizotumiwa na mikoa mingine ili muweze kukamilisha ujenzi huo kwa muda mwafaka.

Ingependeza kama mkoa utakwenda sawa na kasi ya serikali ya kuboresha elimu, hasa ya ujenzi wa sekondari hizo ili kuongeza ufaulu wa masomo ya sayansi na TEHAMA kwa wasichana.