SEHEMU kubwa ya eneo la kituo cha mabasi au stendi ya daladala Mbezi Mwisho jijini Dar es Salaam, imevamiwa kwa nguvu mpya na wamachinga.
Licha ya eneo lote la Mbezi mwisho sasa kujaa vibanda vilivyofunikwa na nailoni, kilio zaidi kipo upande wa chini wa stendi ya mabasi ya kwenda Kinyererezi, Gongo la Mboto na Temeke.
Hapo wafanyabiashara wadogo na wachuuzi wa kila bidhaa wamerundikana kila upande.
Machinga hao wameweka vibanda kando ya barabara hadi kuziba njia ya wanaotembea , kitendo kinachowalazimisha watumiaji wa njia hiyo wapite barabarani wakipigana vikumbuko na magari, pikipiki na bajaji.
Wengine wameweka vibanda juu ya mitaro ya maji ya mvua. Yaani kwa ujumla mazingira wanayofanyia biashara si rafiki bali ni hatari kwao kama hazitachukuliwa hatua za kuwapanga upya.
Kuna haja ya kuchukua hatua kwa sababu ikitokea ajali wanaweza kupoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa au kuumizwa vibaya, kwani mazingira waliyomo hayawafanyi kuwa na tahadhari dhidi ya hatari yoyote.
Wamo katika vibanda vilivyo juu ya mitaro vikiwa vimezibwa na karatasi za nailoni, hivyo wakiwa ndani hawawezi kuona kinachoendelea barabarani, kwa maana hiyo ikitokea ajali, ni rahisi kuwaumiza.
Ukweli ni kwamba mazingira kama hayo, si vyema watu kukaa na kujisahau kama wako nyumbani huku wengine wakielekeza migongo barabarani kana kwamba wapo katika mazingira salama kumbe ni barabarani.
Ukweli ajali haina kinga, lakini kuchukua tahadhari ni jambo la muhimu, kwani ikitokea ajali eneo hilo watu wengi wanaweza kuumia, na huenda lawama zitaelekezwa serikalini na kumbe chanzo watu wenyewe.
Hatua zinazoendelea sasa za kuwapanga upya machinga wa Kariakoo, zingefika hata Mbezi Mwisho, ili kuwaepusha na ajali zinayowanyemelea, ingawa wao wanaweza kudhani kuwa wako salama.
Barabara nyingi za eneo hilo ni nyembamba, magari yanapishana kwa tabu, huku madereva wa bajaji na bodaboda nao kama kawaida wakiendesha bila kuzingatia sheria ya usalama barabarani.
Katika mazingira hayo, madereva wa mgari wanaweza kuwakwepa na kujikuta wamevamia mabanda ya machinga na kusababisha wafanyabiashara waliomo kwenye maeneo hayo kupoteza maisha.
Ikumbukwe, ni rahisi kwao kugongwa, kwasababu wanapokuwa katika mabanda hayo, hawaoni kinachoendelea barabarani, kwa hiyo hata gari likiacha njia na kuwafuata, hawawezi kujua.
Wakati machinga wakiwa katika hatari hiyo, wapo pia wengine eneo hilo, wanaonyemelewa na janga la kugongwa na magari. Hawa ni wale ambao wanavuka Barabara ya Morogoro bila kufuata utaratibu.
Pembeni mwa barabara hiyo, umewekwa uzio ili wapita njia daraja kuvuka upande wa pili, lakini kuna watu hawatumii daraja, badala yake wanapenya katika uzio, kitendo ambacho ni hatari kwao.
Uzio huo umewekwa baada ya barabara hiyo kupanuliwa, ili kuepusha watu kugongwa na magari, lakini wapo baadhi ya watu wasiotaka kufuata hatua zilizochukuliwa na serikali za kuwanusuru dhidi ya ajali.
Kwa hali ilivyo sasa, nikumbushe kuwa ipo haja kwa mamlaka za manispaa, mkoa na za usimamizi wa barabara kuwasaidia watu wa aina hiyo kuacha mazoea hayo na kuzingatia taratibu, kanuni na sheria kuliko kila mtu kufanya anavyojisikia.
Yote hayo ni kuishi kwa mazoea ambayo yanasababisha watu kufanya lolote wanalojisikia, ikiwamo hata kufanya biashara katika maeneo yenye matangazo yanayowataka wasiwepo eneo husika.
Mtindo huo wa 'kuchezea' mazingira hatarishi, uepukwe ili kuwa katika mazingira salama, kuliko kuendelea kuhatarisha maisha yao bila sababu ya msingi.
Inasikitisha kuona daraja la waenda kwa miguu lipo, lakini watu wanavuka barabara kwa kulazimisha kupenya kwenye uzio, ambao umewekwa ikiashiria kuwa kuna njia ya kuvuka eneo husika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED