KUPANDA maua ni njia mojawapo ya kupendezesha mazingira nyumbani, mitaani na mijini. Kutokana na hilo, karibu kila penye maeneo hayo watu wamepanda maua ya aina mbalimbali.
Pamoja na kwamba maua ni mapambo katika miji na nyumbani, tahadhari inatolewa kwamba ni vyema kuwa makini na maua ya kupanda nyumbani ili kuepusha madhara ya kiafya yanayotokana na mimea hiyo.
Msimamizi wa kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu (NPCC), kilichopo Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Yohana Goshashy, anaitahadharisha jamii kuhusu kupanda maua kiholela.
Yohana anasema kabla ya kuchukua hatua za kupendezesha mazingira ya nyumbani, ni vyema kuwaona wataalam wawaoneshe maua ambayo hayana madhara.
Kwa nini? Kwa sababu baadhi ya mimea hiyo inaweza kusababisha mzio kwa watoto, hasa wakigusisha na sehemu kama macho na mdomo, wanaweza kuwashwa macho na midomo kuvimba.
Pia wengine kulazwa hospitalini na hata kupoteza maisha endapo wakitafuna mbegu za maua hatari.
Hivyo jamii inatahadharishwa na kutakiwa kuwa makini kwenye suala la upandaji wa maua nyumbani.
Katika ufafanuzi wake, mtaalamu anasema maua mengi yana majina ya kisayansi na ya Kiswahili au Kiingereza ambayo wengine wanayatumia kwa tiba pia na urembo, akisema mnyonyo na kwamba unaweza kusababisha kifo.
Ni wakati wa wale wanaopenda kupanda maua nyumbani au maeneo wanakocheza watoto kuchukua hatua zinazoshauriwa.
Ni kweli mimea ya maua mbalimbali ni mapambo yanayopendezesha makazi lakini suala la kuchukua tahadhari, kulinda afya ni la muhimu, ili kupanda mimea isiyo na madhara kiafya.
Katika jamii, watu wanajenga nyumba zao na kuzipamba kwa maua mengi yanayonukia, na kumbe ndani ya hiyo harufu nzuri kuna hatari ambayo inaweza kumkuta mpandaji bila kujua.
Hivyo, kwa elimu ya mtaalam huyo, itoshe kutufundisha kitu, ili kama ikiwezekana, tutumie nafasi kubwa kupanda miti ya kivuli na matunda pembeni mwa nyumba zetu badala ya kurundika maua.
Ninaamini kwamba asilimia kubwa ya watu, watakuwa hawana elimu kuhusu madhara yanayotokana na maua, kwani lengo la kupanda ni kutaka kupendezesha mji si kuleta kuumiza familia.
Kwa maana hiyo, kama itawezekana, ninadhani ni vyema jamii ikaelimishwa kwa upana zaidi kuhusu utunzaji wa mazingira ya nyumbani, hasa kwa upande wa upandaji wa maua.
Ni kawaida kwenda katika mji na kukuta umepambwa na maua ya aina mbalimbali, lakini inapokuja taarifa kuwa yapo baadhi ya maua ni hatari kiafya. Hii ni taarifa mpya ambayo ni vyema jamii ikaipata kwa undani.
Iwapo jamii itakuwa na uelewa wa kutosha, itakuwa ni rahisi kutambua maua hatari na yale ambayo hayana madhara, na itakuwa ni rahisi kuyatambua na kuyaepuka haraka.
Vinginevyo, watu wanaweza kuendelea kuumia bila kujua chanzo chake. Lakini wakionyesha maua hatarishi itakuwa ni rahisi kuchukua hatua ya kuachana nayo badala ya ilivyo sasa.
Kinachotakiwa, ni kujua aina ya maua ambayo unayo nyumbani kwako kama kuna yenye sumu uyaondoe haraka iwezekanavyo kabla hayajasababisha madhara kwako au familia yako.
Hiyo inategemea elimu ambayo atakuwa amepewa na wataalam wa mambo ya maua, na kama itashindikana, basi ni vyema watu waelekeze nguvu pia kwenye kupanda mboga.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED