MABORESHO katika sekta ya elimu kuanzia msingi, sekondari hadi vyuo vikuu yamechangia ongezeko kubwa la wahitimu.
Kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia huku serikali ikibeba mzigo wa kutoa ruzuku ya elimu ya msingi bila ada kuanzia darasa ya awali hadi kidato cha sita ili watoto wasome bila vikwazo ni jambo la kujivuniwa.
Na pale wanafunzi hao wanapofanya vyema katika mitihani ya kidato cha sita na hatimaye kuendelea na masomo ya shahada katika vyuo vikuu, serikali imekuwa ikitoa mikopo kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
Haya yote yanafanyika kwa nia njema ya kuhakikisha vijana wa Tanzania wanakuwa na maarifa, ujuzi na stadi stahiki za kuwawezesha kujitegemea.
Moja ya changamoto katika mfumo wetu wa elimu kabla ya maboresho ya mitaala yaliyofanyika ilikuwa ni ukosefu wa ujuzi wa kuwezesha vijana kuajiriwa au kujiajiri wenyewe baada ya elimu zao na wengine hata baada ya kozi.
Ni wazi wahitimu wa kada mbalimbali wamekuwa wakiandaliwa kuajiriwa bila kuwa na stadi na ujuzi wa kujiajiri, hali hii ikapelekea serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kuchukua hatua.
Mikakati ya kuziba udhaifu huu ni pamoja na kufanya maboresho ya mitaala ambapo sasa mafunzo ya amali yanapewa msukumo mkubwa ili kuwajengea uwezo wanafunzi kuwa na ujuzi wa kuwasaidia kujitegemea bila kutegemea ajira rasmi.
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), inachochea maendeleo ya elimu kwa kutoa mikopo, lakini kuwasaidia wanufaika kuwa na ujuzi stahiki ambao utakuwa nyenzo muhimu ya kuajiriwa na kujiajiri na hatimaye kuwa na uwezo wa kurejesha mikopo waliyokopeshwa.
Ni katika muktadha wa kuwajengea uwezo wahitimu ili kuajiriwa kirahisi au kujiajiri, bodi imeandaa mafunzo rasmi ya kuwasaidia wahitimu ili wawe na ujuzi ambao ni mtaji muhimu katika maisha yao, hasa baada ya kuhitimu masomo yao.
Bodi kwa kushirikiana na Taasisi ya Adanian Labs wameandaa mafunzo kwa wanafunzi wa mwaka wa mwisho na wahitimu katika michepuo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHEMA) na Sayansi ya Kompyuta ili kuwawezesha kujiajiri au kuajiriwa, na hivyo kuwa na vipato ambavyo pamoja na kuendesha maisha yao, watachangia maendeleo ya uchumi wa nchi. Vilevile, watakuwa na uwezo wa kurejesha fedha walizokopeshwa wakiwa vyuoni.
Hivyo basi, mbali na kutoa mikopo na kuwadai wanufaika wake, sasa imeamua kujiongeza na kufanya jitihada za kuwatafutia fursa wanufaika wake ili wawe na uwezo wa kurejesha fedha na hatimaye wengine waweze kusoma kupitia marejesho ya fedha zao. Hii ni hatua murua na ya kupongeza sana.
Mafunzo haya muhimu yenye lengo la kuwajengea uwezo wanafunzi wa mwaka wa mwisho na wahitimu wa fani za TEHAMA na kompyuta ambao ni wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu yatasaidia sana kuwaongezea umahiri, stadi na ujuzi ambao ni muhimu sana katika kujitegemea kiuchumi badala ya kubaki nyumbani wakisubiri ajira rasmi kutoka serikalini au katika sekta binafsi.
Ikumbukwe kuwa, mafunzo haya yatatolewa bure kwa njia ya mtandao kwa kipindi cha miezi minne kuanzia wiki hii Agosti 5, 2024. Kwa kuwa, mafunzo haya yataendeshwa kwa njia ya mtandao, kila mwombaji anapaswa kuwa na kompyuta na intaneti ili kuweza kujifunza kikamilifu na kupata ujuzi na stadi muhimu.
Wahitaji wajue kuwa, kwa zama hizi za ushindani katika soko la ajira, mhitimu mwenye ujuzi wa kutosha anajiweka katika nafasi nzuri ya kuajiriwa na kujiajiri na ndiyo maana taasisi mbalimbali zinashauriwa kutoa fursa kwa wahitimu kujitolea katika taasisi zao ili kuwaongezea ujuzi wanafunzi na wahitimu kwani ujuzi huo ni muhimu katika kujitegemea kiuchumi.
Sanjari na hilo, uamuzi wa HESLB kushirikisha wadau wengine kuwajengea uwezo wanafunzi na wahitimu ni wa kupongezwa kwani unasaidia moja kwa moja kupunguza tatizo la ajira kwa vijana wa Tanzania kwa kuhakikisha wanapata ujuzi na stadi zinazoendana na; mazingira na ushindani wa soko la ajira. Kwa wataalamu wa TEHAMA na kompyuta jitokezeni kwani fursa hii si ya kuichezea, ombeni kujiunga na mafunzo haya ili mjiongezee uwezo na ujuzi na hatimaye muwe na uwezo wa kujitegemea kiuchumi na kulipa fedha mlizokopeshwa mkiwa vyuoni kwa maendeleo ya nchi yetu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED