DUNIA ya sasa na Tanzania yetu maradhi hasa yasiyoambukiza kama saratani na changamoto za ini ni mengi na vyanzo vyake vinatajwa.
Licha ya watu kuelezwa kuwa maisha ya kubweteka na ulaji usio na mpangilio unaojaa wanga zaidi kuliko mlo kamili ni tatizo, upande mwingine sumu na kemikali kwenye vyakula zina mchango.
Ulaji wa nafaka zinazohifadhiwa na kutunzwa kwa kemikali za sumu waweza kuwa mwanzo, lakini pia kunyunyizia dawa hizo kwenye mboga na matunda mashambani na bustani vinahusika pia.
Kemikali hizo zinachafua vyakula , maji na ardhi na kuathiri mazingira na ikolojia nzima.
Ni kweli kuna wadudu vamizi waliotokea sehemu mbalimbali duniani kuanzia Amerika hadi Afrika, wanaoshambulia mazao.
Wanaharibu uzalishaji wa mazao ya chakula hadi ya biashara na wamesambaa kila mkoa, na ili kulima na kuvuna kwa tija ni lazima kuwatibu kwa kemikali za sumu.
Wadudu hawa wana athari kubwa wanashambualia mazao hatua zote kuanzia mbegu ,miche, majani, shina, maua na matunda.
Wanakula mboga, nafaka, matunda ya mazao jamii ya nyanya ikiwamo nyanya chungu, hoho mnavu, pilipili aina zote, ngongwe, biringanya na magugu yenye jamii ya nyanya kama ndulele hivyo kusambaa kwa haraka.
Lakini, ni lazima kutafuta dawa. Inapoandaliwa Dira ya Taifa 2050 ni lazima kuweka mkazo wa kuwa na chakula salama.
Mpango uende na kuwa na wataalamu pamoja na na viwanda vya kukizalisha viuatilifu hai vya kupambana na wadudu hao ili kulihakikishia taifa usalama na ulinzi wa chakula.
Ni vyema sasa kuwa na taasisi za kuchochea uzalishaji huo kwa ngazi zote kuanzia vijijini hadi mijini na pia kuwa na maabara kubwa kwa usajili na uchunguzi na kujenga viwanda na uwekezaji mkubwa kwa kushirikisha wawekezaji wenye nia ya kuleta usalama kwenye chakula na kulinda mazingira.
Ni lazima pia kuwaeleza wananchi kutumia dawa za asili ili kuua visumbufu, kurutubisha mimea, kupunguza matumizi ya mbolea za kemikali na kulinda wadudu rafiki kama nyuki ili kuongeza uchavushaji na mavuno.
Mahindi ni zao kuu la chakula likilimwa karibu mikoa yote kuanzia Shinyanga, Kilimanjaro, Tanga, Mwanza, Arusha, Morogoro, Tabora, Pwani, Dar es Salaam, Iringa, Njombe, Mbeya na Manyara.
Lakini kote huko linashambuliwa na visumbufu na kutishia hatma ya zao hilo na upatikanaji wa chakula.
Ni vyema pia Dira ya 2050 iangazie uzalishaji wa viuatilifu hai na mbolea za asili ili kuleta afya na usalama wa chakula na kupunguza matumizi ya kemikali ambazo zinaweza kuathiri bayoanuai na kuua Watanzania.
Ikumbukwe kilimo kina umuhimu wa kipekee kwenye kufikia utoshelevu na usalama wa chakula ni lazima Dira ya 2050 ilete mabadiliko ya kufikia kilimo hai na kuongeza tija katika uchumi endelevu kwa Watanzania.
Ni lazima kuwa na viuatilifu na mbolea hai zisizo na kemikali wala viambata sumu lakini vinavyoua wadudu na kuboresha udongo na mimea pamoja na kuondoa usugu kwa wadudu kwa, mfano zama hizi mahindi yanaposhambuliwa na wadudu unaweza kutumia dawa mara nyingi lakini ghafla wanaibuka tena.
Ni kutokana na usugu hivyo, mkazo uwekwe kwenye viuatilifu asilia ili kuondoa usugu huo ambao unaathiri ikolojia na maisha ya viumbe na wanadamu.
Ikumbukwe wadudu wengi wamekuwa sugu kwenye viuatilifu vya kemikali ambazo ni hatari kwani zinaacha mabaki ya sumu kwenye mazao na ardhini.
Ni lazima pia dira isimamie na kuendeleza uhifadhi wa bayoanuai na teknolojia zinazotunza mazingira kwa uendelevu ambazo ni za asili.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED