TANZANIA wala si kijiji kilichojitenga hapa duniani, badala yake wananchi wanafuatilia matukio na mambo yote yanayotokea ulimwenguni.
Katika nyanja ya soka, tumekuwa tukiona michezo mkubwa, hasa timu za mahasimu wa nchi au mji mmoja katika mabara mbalimbali duniani zikichezeshwa na waamuzi kutoka nje ya nchi.
Miaka inavyozidi kusonga mbele kwa soka kuwa biashara kubwa, kumekuwa na uhitaji mkubwa wa uwazi wa uhitaji wa waamuzi kutoka nje ya nchi kwenda kuchezesha michezo maalum, ambayo ni ile yenye mvuto kwa mashabiki na mikubwa.
Kwa sasa tunaona dabi kubwa Brazil, Argentina na kwingineko ambako soka limepiga hatua kubwa, zimekuwa zikileta waamuzi kutoka nje ya nchi ambao kazi yao inakuwa ni kuchezesha michezo hiyo tu na wanarudi kwao.
Hapa Afrika, dabi mbalimbali za Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Rwanda, Misri, Morocco, Tunisia na nyinginezo zimeshaanza kuleta waamuzi kutoka nje kwa ajili ya dabi zao.
Tanzania ambayo ni ya sita kwa ubora wa Ligi Kuu Afrika, bado imeendelea kutumia waamuzi wake wa nyumbani kwa ajili ya michezo hiyo huku kila wakati wakivurunda na kupoteza ladha ya dabi.
Ingeeleweka kama kusingekuwa na matatizo kwenye uchezeshaji wao, lakini kila mechi wanazochezesha zimekuwa na matatizo. Na ukiangalia tatizo la waamuzi wa Tanzania ni woga wa kufanya maamuzi katika matukio yanayotokea dhahiri uwanjani kwa kukwepa lawama na si vinginevyo.
Hili ndilo limesababisha nchi nyingi kuanza kuleta waamuzi kutoka nje ili kuchezesha dabi zao. Zimegundua kuwa wakati mwingine wala si mapenzi ya mwamuzi au rushwa, ila waamuzi ni sehemu ya raia wa nchi hiyo, hivyo anaweza kufanya maamuzi kwa ajili tu ya kujilinda ili aishi kwa amani mtaani.
Kwa maana hiyo hawezi kufanya baadhi ya maamuzi magumu ambayo anaona yanaweza kumfanya asakamwe na kulalamikiwa.
Nadhani hili sasa lianze kuangaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) na bodi yake, kuanzia sasa mechi kubwa, zenye mvuto na kutawalia na hisia kuchezeshwa na waamuzi kutoka nje ya nchi.
Kabla ya kumalizika kwa msimu uliopita, TFF ilisema kuna waamuzi kutoka Sudan wapo nchini na wengine walionekana kuchezesha baadhi ya michezo, hasa wale wa pembeni, sasa nadhani imefika wakati wa kuwaleta wengi zaidi kwa ajili hiyo.
Waamuzi wa Sudan ambao kwa sasa hawachezeshi ligi kutokana na nchi yao kukumbwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe, wangeweza kupewa fursa hiyo kuliko Watanzania wenyewe ambao wengine wao wamekuwa wakijirudia kuchezesha mechi hizo, huku wakigawana makosa, kwa sababu kutokana na mara nyingi malalamiko kujitokeza.
Labda nielezee faida za waamuzi kutoka nje wakichezesha dabi. Moja ni kwamba wataaminika na timu zote mbili. Ule ugeni wao ni faida, kwani kwa hisia za timu zote mbili ni kwamba kama anatoka nje ya nchi hatokuwa na mapenzi ya upande wowote. Pili hisia za mashabiki wa Simba na Yanga zitaona si rahisi kula mlungula kwa sababu ni waamuzi wa kimataifa.
Tatu, waamuzi hawa wanaweza kufanya maamuzi magumu na sahihi kwa muda wowote bila kuhofia chochote, kama kusemwa mitaani, kwenye vyombo vya habari, wachambuzi, kwa sababu akishamaliza yeye anaondoka kwenda kwao.
Nne ni kwamba atawafanya hata wachezaji kuwa na nidhamu kwa sababu wanajua ni mwamuzi kutoka nje, moja ya sababu ambazo waamuzi wetu wanapata tabu ni kwamba wachezaji wameshawajua kuwa ni waoga, hivyo wanawatisha na kuwazonga mara kwa mara, licha ya kwamba ni kweli wamefanya makosa.
Na hizi ndizo faida ambazo nchi nyingi kwa sasa wanaowatumia waamuzi kutoka nje kwenye dabi zao, wanazitapa.
Ligi ya sita kwa ubora Afrika, inatakiwa sasa ijiongeze kwa kuleta waamuzi kutoka nje, ili pia kuwalinda waamuzi wa ndani kwa lawama ambazo wakati mwingine zinawafanya wasijiamini.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED