WIKI ilikuwa ya moto sana kwenye mitandao ya kijamii na vipindi vya michezo, hasa baada ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo kuja na maelezo ya kuwachukulia hatua wasemaji wa klabu au Maofisa Habari ambao wanachekesha, badala ya kuwahabarisha wanamichezo nini kinaendelea katika klabu zao.
Ofisa Mtendaji Mkuu yeye akataka wasemaji kujikita kwenye kuelezea timu zao ‘kavu kavu’ bila kuonesha chembe ya ucheshi.
Jambo hili limezua mjadala sana kwa wanamichezo, na hata ambao si wanamichezo, yaani watu wa kada nyingine wakijiuliza kama Bodi ya Ligi itawachukulia hatua watu hao, itakuwa inatumia vigezo gani kutambua kama msemaji huyo amechekesha, au waaandishi wa habari na wasikilizaji wamecheka bila yeye kuchesha.
Sijajua sana lengo hasa ilikuwa ni nini, au alikuwa anamaanisha haitakiwi kabisa kwa Ofisa Habari kuchekesha au kufanya mizaha, lakini nadhani binafsi naona kulikuwa na mambo mengi muhimu kwa Bodi ya Ligi kutolea ufafanuzi kuliko hilo ambalo halina tija.
Kwanza kabisa ucheshi au kuchekesha ni kipaji, wala siyo kila mtu anaweza kuwafurahisha watu, si kwa Maofisa Habari na Wasemaji, bali hata kwa Wanasiasa.
Sasa sidhani kama kweli Kasongo alikuwa anazuia kipaji cha mtu. Mwingine hata asipochekesha, jinsi anavyoongea tu na kuwasilisha taarifa au ujumbe wake watu anajikuta wanacheka.
Nitoe mfano kwa Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, ni kiongozi ambaye Dunia nzima inamfahamu kuwa ni mmoja wa viongozi bora kuwahi kutokea.
Amefanya mambo mengi mazuri ambayo yameendelea kukumbukwa vizazi hadi vizazi. Lakini ukimsikiliza kwenye hotuba zake zote, hakuna hata moja ambayo Waandishi wa Habari na wengine wanaomsikiliza'hawajavunjika mbavu.'
Ni hotuba bora kabisa zenye msisimko, hekima na busara za hali ya juu, lakini karibuni zote zimebebwa na ucheshi, kiasi kwamba watu wanaweza kukaa wanasikiliza hata masaa manne bila kuchoka kumsikiliza au mtu kusinzia.
Rais wa awamu ya tano, John Magufuli, naye alikuwa na aina fulani ya hotuba za ucheshi, ambazo ziliwaacha wasikilizaji wakifurahi na kucheka, huku wakiendelea kumsikiliza.
Hii ni mifano michache ya Wanasiasa ambao wana uwezo huo, hiki ni kipaji na si kila mtu anaweza.
Hata kwa watu wa kawaida, utakuta kuna mtu ukikaa naye unafurahi tu kutokana aina yake ya mazungumzo na uwasilishaji wa maneno yake, halafu mwingine hana kipaji hicho.
Kwa wasemaji, kuna mtu anaitwa Thobias Kifaru, Masau Mbwire, Ahmed Ally na wengineo ni baadhi ya wasemaji wanaoonekana wana vipaji vya kuwasilisha taarifa zao kwa namna ya ucheshi na wamekuwa hivyo kwa miaka mingi na watu wamekuwa wakifurahi wanapowasikia wakiongea. Hilo huwezi kuondoa kwa sababu ni kipaji kutoka kwa Mungu. Hata ukiwaiga huwezi. Lakini sijawahi kusikia wakimdhalilisha au kumsema mtu kwa kuukweza utu wake kwa sababu ya mpira.
Tujiulize, kama hata viongozi walikuwa watoa hotuba zao zenye ucheshi ndani yake, iweje kwenye mpira tu ambao ni burudani ndiyo ikatazwe?
Mimi nadhani Kasongo angetuambia kuwa anapiga marufuku Maafisa Habari ambao badala ya utani, wanadhalilisha klabu zingine kwa kuchafua 'brandi' kwa kisingizio cha utani wa jadi, kumshambulia mtu binafsi kwa maneno au taasisi.
Utani, masihara, ucheshi ndivyo vinavyonogesha mpira wetu, hivi vingeachwa tu, na badala yake Bodi ya Ligi ingejikita kwa wale wenye lugha za zenye ukakasi kwa wenzao, kuvunjiana heshima, vitu ambavyo tumekuwa tukiviona.
Na hili lifanyike si kwa kuchagua au kumuangalia mtu usoni, adhabu itolewe kwa yoyote atakayefanya, ila hili la 'vichekesho', sidhani kama lina maana sana.
Bodi simamieni misingi ya uadilifu wa heshima, adabu, hivi ndivyo muhimu zaidi kuliko hilo la ucheshi wa maneno.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED