Stars: Nafasi kufuzu AFCON bado tunayo

By Adam Fungamwango ,, Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 10:42 AM Oct 17 2024
 Kaimu Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Hemed Suleiman 'Morocco'.
Picha:Mtandao
Kaimu Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Hemed Suleiman 'Morocco'.

WAKATI Kaimu Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Hemed Suleiman 'Morocco' akisema Tanzania bado ina nafasi ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2025), wapinzani wao Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo), waanika walikuwa wanamhofia zaidi nyota, Simon Msuva.

Taifa Stars ilikubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa DR Congo ambayo ni kinara wa Kundi H ilifikisha pointi 12 inafuatiwa na Guinea yenye pointi sita baada ya kuichapa Ethiopia mabao 3-0 na Stars iko katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi nne kibindoni.

Mabao yote mawili ya DR Congo yalifungwa na nyota anayechezea Young Boys ya Uswizi, Meshack Elia, ambaye aliingia akitokea benchi.

Akizungumza baada ya mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kumalizika, Morocco alisema hawajakata tamaa ya kufuzu AFCON na anawasihi Watanzania kutovunjika moyo kwa sababu kufungwa mchezo huo wa juzi si mwisho wa safari yao.

Morocco alisema sababu kubwa iliyopelekea kupoteza mchezo huo wa jana ilitokana na viwango vya mchezaji mmoja mmoja kwa timu hizo mbili.

Kocha huyo alisema pamoja na wachezaji wake kujitahidi 'kutoa jasho lao lote' uwanjani, lakini walihukumiwa na ukosefu wa umakini dakika za mwishoni.

"Viwango vya mchezaji mmoja mmoja vimefanya matokeo kuwa kama yalivyokuwa. Ukiangalia katika mchezo huu tumecheza vizuri, hasa kipindi cha kwanza tumejaribu kutengeneza nafasi, bahati mbaya hatukuzitumia, wenzetu walivyorejea kipindi cha pili walijaribu kusukuma mashambulizi mengi kwetu, tulilazimika kuumiliki mpira kadri muda ulivyozidi kwenda, lakini dakika za mwisho ukosefu wa umakini, umesababisha tumepoteza mechi," alisema Morocco.

Hata hivyo aliwapongeza DR Congo kwa jinsi walivyocheza na hiyo imetokana na kikosi chao kuundwa na wachezaji wazuri kwenye uwezo wa kuamua mechi, ingawa hilo halikuwafanya nyota wake kuvunjika moyo, watapambana mpaka dakika za mwisho.

"Niwapongeze DR Congo walikuwa na wachezaji wazuri waliokuwa na uwezo wa kuamua mechi, lakini kwetu sisi safari inaendelea, bado tuna nafasi ya kusonga mbele, tumefungwa, ila si mwisho wa safari, tunaweza kupata nafasi ya kujirekebisha," Morocco aliongeza.

Naye mshambuliaji wa DR Congo, Fiston Mayele, alisema sababu iliyowafanya wapate ushindi ni kuizidi mbinu na ubora Taifa Stars.

Mayele alitaja sababu nyingine iliyowapata pointi sita dhidi ya Taifa Stars ni kukosekana katika kikosi hicho, winga wa kimataifa, Simon Msuva.

"Tulikuwa tuna hofu sana na Msuva pamoja na Samatta (Mbwana), hata kocha wetu alikuwa anafuatilia nani na nani wataitwa kwenye Timu ya Tanzania, Msuva ana kasi na anajua kukimbia kwenye 'space' (nafasi), kama angekuwa na Samatta pale mbele tungekuwa kwenye hatari zaidi, sijui ni kwanini hajaitwa," alisema Mayele.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga alisema Samatta alikuwa ni mchezaji wanayemhofia zaidi kwenye mechi zote mbili walizocheza.

"Amecheza vizuri sana katika mechi zote, anajua kukaa na mpira na ni mgumu kumpokonya, nadhani kama angekuwa na Msuva kazi kwetu ingekuwa ngumu kidogo, lakini tumefurahi kupata ushindi na kufuzu AFCON," alisema nyota huyo ambaye kwa sasa anakipiga katika Klabu ya Pyramids ya Misri.

Beki wa kati wa DR Congo, Henock Inonga, alisema Stars ilicheza vizuri kwenye michezo yote miwili lakini wao walikuwa wazuri katika kutumia nafasi walizozipata.

"Mchezo ulikuwa mzuri sana, Tanzania wamecheza vizuri na kumiliki mpira hasa kipindi cha kwanza, lakini tumewazidi kwenye mbinu na kutumia nafasi," alisema Inonga.