Singida yanogewa kileleni Bara, yaitambia Namungo

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:47 AM Oct 17 2024
SINGIDA Black Stars
Picha: Mtandao
SINGIDA Black Stars

SINGIDA Black Stars imesema imeshaonja 'utamu' wa kukaa kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Bara hivyo haitakuwa rahisi kushushwa kwa sababu wanataka kuendelea kung'ang'ania kwenye nafasi hiyo kwa kupata ushindi watakapocheza dhidi ya Namungo Jumapili kwenye Uwanja wa Liti mkoani, Singida.

Singida Black Stars iko kileleni ikiwa na pointi 16 lakini imecheza michezo mingi zaidi ikifuatiwa na Simba yenye pointi 13 sawa na Fountain Gate FC huku mabingwa watetezi, Yanga yenye pointi 12 wakiwa nafasi ya nne.

Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza, amesema jana, wamepata bahati kubwa ya kukaa kwa muda mrefu kileleni huku ligi ikisimama kutokana na Kalenda ya Kimataifa, wanataka kubakia kwenye nafasi hiyo na wataonyesha vitendo kwa kuwafunga Namungo.

"Tunashauku ya kuhakikisha tunaendelea kuongoza ligi kwa muda mrefu na hata hadi mwisho wa msimu, tumekuwa huko tangu mapumziko ya kalenda ya FIFA, hiyo ni hamasa tosha kwa wachezaji, tumeshawaambia kukaa namba moja si kazi, kuhakikisha tunaendelea kukaa pale ndiyo kazi kubwa," alisema Massanza.

Alitamba wamejipanga vyema kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo ili kutengeneza wigo kwa timu nyingine ambazo zinawakimbiza.

"Tunajiandaa kwenda kutafuta pointi tatu dhidi ya wageni wetu Namungo, tutacheza kwenye uwanja wa nyumbani hivi sasa maandalizi yanaendelea," Massanza alisema.

Singida Black Stars ambayo imeshinda mitano na sare moja, ikifunga magoli tisa na kuruhusu nyavu zake kuguswa mara tatu.

Timu hiyo pia inaongoza kwa kuzoa pointi nyingi zaidi kuliko timu yoyote ya Ligi Kuu ikicheza viwanja vya ugenini, ikijizolea pointi 12, ambapo imecheza michezo minne nje ya nyumbani kwake, Liti Singida, ikishinda yote, huku michezo miwili ya nyumbani ikishinda mmoja na sare moja.