Simba yatamba kuonesha ukubwa CAF

By Faustine Feliciane ,, Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:15 AM Jul 13 2024
Wachezaji wa Simba wakiendelea na mazoezi yao ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu na michuano ya kimataifa katika jiji la Ismailia nchini Misri.
PICHA: SIMBA
Wachezaji wa Simba wakiendelea na mazoezi yao ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu na michuano ya kimataifa katika jiji la Ismailia nchini Misri.

SIKU moja baada ya droo ya michuano kombe la Shirikisho Afrika kupangwa, uongozi wa klabu ya Simba umesema umepokea kwa furaha ratiba ya michuano hiyo kwa kuwa wanaenda kukutana ma timu ambazo zipo chini yao kiuwezo kwenye hatua ya kwanza.

Katika droo iliyochezeshwa makao makuu ya CAF, Cairo, Misri, Simba ambayo itaanzia hatua ya kwanza, inasubiri kucheza na mshindi kati ya Uhamiaji FC ya Zanzibar na muwakilishi kutoka Libya ambaye bado hajajulikana kwenye mchezo wao wa hatua ya awali.

Meneja wa habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally aliiambia Nipashe kuwa njia kwao ni nyeupe kusonga mbele kwenye michuano hiyo.

"Tumepokea vizuri droo ya CAF, hatuwadharau wapinzani, yoyote atakayekuja tunadili naye, kwetu tunaona njia nyeupe kwenda hatua nyingine, tunasubiri mpinzani wetu aje na tutampokea," alisema Ahmed.

Alisema kwa timu yoyote itakayofuzu kwenda kucheza nao, hawatamdharau kwa kuwa ni timu ndogo kwao kwa sababu mchezo wa mpira ni mchezo wa makosa.

"Hizi timu ndogo hatupaswi kuzidharau, ukizidharau wanaweza kukuvua nguo ukweni, kwa hiyo tunajiandaa vizuri, kama mnavyojua tayari timu imeanza maandalizi ya Ligi Kuu pamoja na michuano hii," alisema Ahmed.

Alisema kwa sasa kazi inaendelea kukiandaa kikosi chao kuelekea kwenye msimu mpya wa mashindano.

"Mazoezi yanaanza kupamba moto kwenye kambi  yetu, kila mchezaji ana morali ya hali ya juu, na kocha wetu mpya Fadlu Davids amefurahishwa na hali aliyoikuta kwa wachezaji wake," alisema Ahmed.

"Kusema kweli kocha ameshaanza mazoezi na ameonesha kufurahishwa na viwango vya wachezaji aliowakuta na kusema ana kazi ya kukiunganisha ili kucheza katika mfumo anaouhitaji."

Wakati huo huo, klabu hiyo imetangaza kumsajili beki wa kulia Kelvin Kijili, kutoka klabu ya Singida Fountain Gate.

Kijili amejiunga na klabu hiyo kwa mkataba wa miaka miwili na kazi yake kubwa itakuwa kwenda kuungana na Shomari Kapombe upande wa kulia wa kikosi hicho.

"Tumefanikiwa kuinasa saini ya mlinzi wa kulia wa Singida Fountain Gate kwa mkataba wa miaka miwili,” ilisema taarifa ya Simba.

Kijili mwenye umri wa miaka 24 ni kijana mwenye kipaji na kasi amekuwa akitumika kuanzisha mashambulizi kutokea upande wa kulia na msimu uliopita amesaidia timu yake ya zamani pasi za mwisho, 'asisti' nne.

Wanachama na mashabiki wa Simba kwa misimu mitatu sasa wamekuwa wakilalamika Kapombe na Mohamed Hussein 'Tshabalala' kutokuwa na mbadala.

Ujio wa mchezaji huyo na Mburkina Faso, Valentin Nouma, beki wa kushoto kutoka FC Saint Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, umeonekana kuwafurahisha.

Simba imeweka kambi ya wiki tatu kwenye jiji la Ismailia nchini Misri kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu na michuano ya kimataifa.

Kikosi cha Simba kinatarajiwa kurejea nchini siku chache kabla ya kilele cha tamasha la kila mwaka la klabu hiyo 'Simba Day' litakalofanyika Agosti 3 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa.