Serikali yawaangukia wadau kuelekea CHAN, AFCON 2027

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 05:12 AM Jan 16 2025
Naibu Waziri Mkuu na Waziri Nishati, Doto Biteko.
Picha:Mtandao
Naibu Waziri Mkuu na Waziri Nishati, Doto Biteko.

SERIKALI imewataka Watanzania kuiunga mkono Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars) ili iweze kutwaa ubingwa wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), ambayo sasa yatafanyika Agosti, mwaka huu.

Pia serikali imewataka wadau kutoa sapoti kwa timu yao pale itakapochuana katika  Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), zitakazofanyika Tanzania, Kenya na Uganda. 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri Nishati, Doto Biteko, alisema hayo katika kongamano la wadau mbalimbali wa michezo kuelekea maandalizi ya CHAN 2024 pamoja na  AFCON 2027.

Biteko alisema ili kufikia malengo, Serikali imejipanga vyema kuhakikisha Taifa Stars  inafika mbali katika mashindano hayo kama nchi mwenyeji. 

"Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kuhakikisha Tanzania inanufaika kupitia mashindano ya CHAN yatakayofanyika mwaka huu, pamoja na yale ya AFCON yatakayofanyika mwaka 2027,  yatatumika kuinua uchumi wa nchi yetu," alisema Biteko. 

Pia kiongozi huyo alimshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya katika sekta ya michezo ambayo imezaa matunda makubwa mpaka nchi yetu kupata fursa ya kuwa wenyeji wa mashindano hayo. 

Naye Naibu Waziri wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma, alisema licha ya mashindano ya CHAN kusogezwa mbele, maandalizi yalikuwa yamekamilika kwa asilimia 99.

"Miezi sita tuliyonayo kwa sasa itatusaidia kufanya maandalizi zaidi yatakayoifanya  timu yetu kufanya vizuri, kupitia kongamano hili naamini ushindani utazidi kuwa mkubwa," alisema waziri huyo.

Aliipongeza Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi CHAN na AFCON kutokana na kazi nzuri wanayofanya ili Tanzania ifanye vizuri na kuzidi kuipeperusha vyema bendera ya nchi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, ambaye ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alisema gharama ya kuandaa mashindano kama hayo makubwa ni zaidi ya Sh. trilioni moja.

"Serikali imefanya kazi kubwa kuimarisha miundombinu yote ambayo itatumika katika mashindano hayo mwezi huu, tunatarajia kuongeza viti 20 na vingine vitaletwa ifikapo Machi," alisema Msigwa. 

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema yupo katika mchakato wa kukamilisha miundombinu ya barabara na kuboresha ulinzi ili mpaka ikifika Agosti, mkoa uwe na mvuto mkubwa kwa sababu watakuja wageni kutoka mataifa mbalimbali. 

Wilfred Kidao, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), amesema wamefanya maandalizi zaidi ya mwaka mmoja wakiwa na lengo la kuona Tanzania inaweka historia kwa kufika mbali. 

"Kutokana na maandalizi tuliyoyafanya tunaamini tutaingia fainali katika mashindano hayo," alisema Kidao.