Kamishna Nishati Jadidifu afunguka undani timu ya Samia ilivyojipanga

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:17 PM Jan 15 2025
    Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Innocent Luoga.
Picha: Mtandao
Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Innocent Luoga.

KATIKA wiki moja na nusu ijayo, Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu nishati, ikikusanya viongozi wa nchi 54 wa Bara Afrika.

Pia, wamo Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Umoja wa Afrika (AU), hali kadhalika mawaziri wa fedha, wanaohusika na nishati. 

Katika tukio hilo litakalofanyika kuanzia tarehe 27 hadi 28, mwezi huu katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), washiriki wengine ni mabalozi, wakuu wa taasisi za kifedha za kimataifa, mazingira, nishati na sekta binafsi.

 Hapo mwenyeji nchini kutaaluma serikalini, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu nchini, Innocent Luoga, ana ufafanuzi wake katika jambo hilo: “Tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuipa kipaumbele Sekta ya Nishati, juhudi ambazo zimeonekana kwa nchi na taasisi mbalimbali za kimataifa. 

“Mfano hai ni kufanyika kwa mkutano huu (M300) mkubwa unaowakutanisha wakuu wa nchi zote za Afrika na wengine kutoka mataifa ya Ulaya. 

Hili ni suala la kujivunia kwa Tanzania na tunapaswa kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wetu kwa maono haya makubwa.” 

SABABU ZA MKUTANO 

Katika ufafanuzi wake kwa wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki iliyopita, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Innocent Luoga, anasema: 

 “Takwimu zinaonyesha kuwa takribani Waafrika milioni 685 hawajafikiwa na huduma ya umeme hadi sasa kati ya Waafrika zaidi ya bilioni moja.

 “Kutokana na hilo Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo Afrika wamekuja na mpango mahsusi ujulikanao kama ‘Mission 300’ (au M300) ambao umelenga kuharakisha upatikanaji wa umeme kwa Waafrika milioni 300 ifikapo 2030. 

 “Mpango huu unahusisha nchi zote za Afrika, nchi 14 zimechaguliwa kuanza utekelezaji wa mpango huu na nchi nyingine zitafuata. Kiwango kidogo cha upatikanaji wa umeme kilikuwa ni kigezo kilichotumika.

 “Nchi hizo ni Tanzania, Mali, DRC (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo), Ivory Coast, Bukina Faso, Chad, Liberia, Madagascar, Malawi, Mauritania, Mozambique, Niger, Nigeria na Zambia.

 “Tanzania kwa upande wake itasaini mpango huo kwa kuwa ni nchi mwenyeji wa mkutano kwani imeshapiga hatua kubwa katika usambazaji wa umeme kwa wananchi,” anasema Luoga.

 NAFASI YA TANZANIA

 Kamishna Luoga anaelekeza pongezi kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuipa kipaumbele sekta ya nishati, juhudi zikionekana kitaifa na kimataifa.

 Hapo anarejea mfano wa kukubalika kwa taifa kufanyika mkutano ujao unaowakutanisha wakuu wa nchi za Afrika na viongozi wa nje ya bara hilo.

 Hata juzi katika mkutano wake wa kufungua mwaka na mabalozi wa kigeni waliko nchini Jumanne wiki hii, Rais Dk. Samia akarudia tena hilo kuwa ni sehemu ya mafanikio yanayoshuhudiwa kitaifa, ikiangazwa katika eneo hilo la nishati.

 Hadi sasa kitaifa, mbali na nishati za asili katika vyanzo vya maji kama vile Kidatu, kuna mradi mkubwa Bwawa la Mwalimu Nyerere linalotarajiwa kumaliza shida ya umeme nchini, hata kuuza kimataifa.

 Maeneo mengine yanayojumuisha kupata na kutumia nishati ya gesi nchini, kazi inayoendelea, huku huduma za usambaji nisahati umeme ukifanikiwa kwa kiwango kikubwa, chini ya wakala wake maalum iliyoundwa (REA).

 Wakati inapokea pesa za mradi kutoka Benki ya Dunia mnamo Novemba 2023, REA iliahidi itaiwezesha kuifikia dhamira yake ya kuvipata vijiji 12,318 vilivyolenga kitaifa ifikapo Juni 2024.

 Hiyo ni kwa mujibu wa kauli ya REA wakati huo, mafanikio yakiwa mbele ya dhamira ya kipindi kilicholengwa, 2025, kwamba asilimia 70 ya Watanzania walio vijijini wafikiwe na huduma ya umeme.

 Kuhusu namna taifa limejipanga kunufaika na mkutano huo wa nishati unaotarajia kuanza, Kamishna Luoga anataja orodha ya mikakati kama ifuatavyo;

 Mosi, ni kuvishirikisha vyombo vya habari katika utoaji taarifa na uelewa kuhusu Mpango wa ‘Mission 300’ unatarajiwa kuanza.

 Pili, anataja suala la kuunda timu ya wataalamu wakataondaa Mpango Mahususi wa Kitaifa uitwao ‘National Energy Compact.’ 

Tatu, inatajwa suala la kuzishirikisha tasisisi za umma na binafsi (nafasi ya PPP), pamoja na wadau wa nishati kuhusu mpango huo, ili kupata maoni.

 Nne inatajwa, ni nafasi ya kuainisha na kuandaa miradi itakayowezesha utekelezaji hup wa ‘Mission 300’ nchini.

 Tano, Kamishna na anataja ni suala la kuandaa safu ya wataalamu watakaosimamia utekelezaji wa mpango huo; na mwisho ni namna ya kushirikiana na taasisi za kifedha katika kufuatilia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji. 

 WITO WAKE 

Kamishna Luoga ana wito kuhusu ustawi wa mkutano huo, akiugawa katika maeneo kadhaa, kuanzia na wanahabari akiwasihi fursa yao kitaaluma kuelimisha kuhusu mkutano huo wa nishati, siku 11 zijazo.

 “Napenda kuchukua nafasi hii kuwaomba wanahabari wote kuwa kioo cha nchi, kwa kuutangaza sana mkutano huu na kutoa habari sahihi na kwa wakati,” anatamka.

 Pia, anawarejea wananchi wote, akiomba ukarimu wao kwa wageni, kama ilivyo desturi ya Kitanzania, ndani ya kipindi chote cha mkutano huo ujao wa M300.