Wakulima wanawake 525 kutoka kata 20 za Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga, wameuziwa majembe ya kuvutwa kwa ng’ombe (plau) kwa Sh.50,000 badala ya Sh.200,000 ya bei ya soko. Hatua hii inalenga kupunguza gharama za zana za kilimo na kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Majembe hayo yametolewa na Shirika lisilo la kiserikali la Dorfra Co. Ltd kwa kushirikiana na Shirika la Meda, likilenga kuongeza thamani ya zao la mpunga na kuinua uchumi wa wakulima wanawake kwenye familia zao.
Meneja wa Shirika hilo, Bakari Juma, amesema kuwa kuanzia Novemba 27 hadi 29 mwaka jana, waliwafundisha wakulima hao mbinu za kilimo cha kisasa. Mafunzo hayo yalihusu kanuni bora za kilimo, matumizi ya mbegu bora, utayarishaji wa shamba, matumizi sahihi ya mbolea, udhibiti wa magugu kwa dawa, na kupanda kwa kufuata mstari.
Juma amesema wanawapatia wakulima majembe ya kuvutwa kwa ng’ombe kwa gharama ya Sh.50,000 badala ya Sh.200,000 ya sokoni ili kuongeza uzalishaji wa mazao. Aidha, aliwasihi wakulima kutumia majembe hayo kwa matumizi yaliyokusudiwa na kuepuka kuyauza au kuyakodisha.
Mkuu wa Divisheni ya Kilimo na Uvuvi wa Manispaa hiyo, Pendo Matulanya, amewahimiza wakulima kuwashirikisha maafisa ugani waliopo kwenye kata zao ili kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu utunzaji wa mashamba, mbinu za kisasa za kilimo, na muda sahihi wa kutumia mbolea, hatua itakayosaidia kuongeza mavuno.
Mkulima wa kata ya Mondo, Neema Maziku, amesema gharama kubwa za zana bora za kilimo zimekuwa kikwazo kwao. Hali hii inawalazimisha kulima maeneo madogo, hivyo kupata mavuno ya kujikimu kwa chakula tu. Neema, mwenye zaidi ya ekari sita, amesema kila msimu amekuwa akilima ekari mbili pekee kutokana na changamoto hizo.
Awali, akikabidhi majembe hayo, Mbunge wa Kahama, Jumanne Kishimba, alisema serikali inajitahidi kutengeneza mazingira bora ya kuendeleza sekta ya kilimo ili iwe na manufaa kwa wakulima. Kuhusu gharama kubwa za zana za kilimo, alisema atalifikisha suala hilo kwa Waziri mwenye dhamana ili kuangalia uwezekano wa kuweka ruzuku kama ilivyo kwa pembejeo.
Mbunge huyo pia alishauri shirika hilo kuanzisha mashindano ya uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara ambapo mshindi apewe zawadi kama zana za kilimo, mbolea, au mbegu. Alisema hatua hiyo itahamasisha wakulima wengi kujitokeza na kuongeza uzalishaji, hivyo kuhakikisha uhakika wa chakula kwenye familia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED