Mabusha na matende bado ni tatizo Kinondoni

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 03:50 PM Jan 15 2025
Dk.Peter Nsanya Mganga Mkuu Manispaa ya Kinondoni.
Picha: Pilly Kigome
Dk.Peter Nsanya Mganga Mkuu Manispaa ya Kinondoni.

HALMASHAURI ya Kinondoni inatarajia kuanza zoezi la kugawa kinga tiba kwa wakazi wake katika kata 10 korofi ambazo bado zina maambukizi ya magonjwa ya matende na mabusha kwa wanawake na wanaume.

Katika zoezi hilo, wanatarajia kuwafikia wananchi wapatao 284,036 ambapo walengwa ni wananchi wote kuanzia miaka mitano na kuendelea.

Hayo yamesemwa Januari 14, Mkoani Kinondoni na Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Dk. Peter Nsanya, katika semina elekezi iliyokutanisha waandishi wa habari kuhusiana na magonjwa hayo.

Dk. Nsanya amesema kampeni hiyo ya ugawaji kinga tiba itafanyika kuanzia Januari 22 hadi 26, na itatekelezwa nyumba kwa nyumba, kwenye mikusanyiko, shuleni, vituo vya usafiri, masoko, pamoja na kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kuwafikia watu wote.

Naye Afisa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yasiyopewa Kipaumbele (NTDCP) kutoka Wizara ya Afya, Anna Joseph, amesema jumla ya wilaya 114 zimefanikiwa kuondoa maambukizi ya magonjwa hayo nchini kati ya wilaya 119 zilizokuwa na maambukizi, na kubakiwa na Halmashauri tano pekee ambazo bado zina maambukizi hadi sasa.

1

Joseph amesema Halmashauri hizo ni pamoja na Kinondoni, Mtwara Mikindani, Lindi Manispaa, Mtama, na Pangani.

Kufuatia maambukizi hayo, Serikali kupitia Wizara ya Afya tayari ina mpango mkakati wa kuanza kuzifikia Halmashauri hizo korofi. Wataanza kutoa kinga tiba kwa wananchi wa Halmashauri ya Kinondoni kwanza na baadaye kuzifikia zingine.

Kwa upande wa Kinondoni, maambukizi yamebaki katika kata kumi ambazo ni Kigogo, Mzimuni, Magomeni, Ndugumbi, Tandale, Kijitonyama, Kinondoni, Hananasifu, Mwananyamala, na Makumbusho. Kati ya hizo, Tandale bado ni kinara kwa kuwa na maambukizi ya asilimia 2.3 ukilinganisha na zingine.

Kwa upande wake, Mratibu wa Miradi ya Kuondoa Magonjwa ya Matende na Mabusha kutoka Ofisi ya Mkoa wa Dar es Salaam, Alex Mkamba, alisema zoezi hilo la ugawaji kinga tiba lilianza mwaka 2019 na halina madhara kwa mtumiaji wa kinga hiyo. Amebainisha kuwa kinga hiyo inaweza kumezwa kabla au baada ya kula na haina athari yoyote.

2