KLABU ya Prisons imesema mapumziko ya Kalenda ya Kimataifa kuweka kambi yake jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa na michezo ijayo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, imeelezwa.
Ligi Kuu Tanzania Bara imesimama kupisha michezo ya kimataifa, huku wachezaji wengi wakitimkia katika vikosi vya timu zao za taifa vinavyosaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), zitakazofanyika mwakani nchini, Morocco.
Mtendaji Mkuu wa Prisons, John Matei, ameliambia gazeti hili kikosi cha timu hiyo kitaanza mazoezi yake rasmi kesho baada ya wachezaji kumaliza mapumziko ya siku sita.
Matei alisema baada ya kuifunga KenGold bao 1-0 Jumapili iliyopita, waliamua kuwapa wachezaji wao mapumziko mafupi kwa sababu mechi yao inayofuata dhidi ya JKT Tanzania itachezwa Novemba 24, mwaka huu.
"Baada ya kumaliza mechi ya KenGold tulivunja kambi na kuwapa vijana mapumziko ya kama wiki moja au siku sita hivi, Novemba 9 (kesho) wanatakiwa kurejea kambini kujiandaa na michezo ijayo, kambi yetu kama kila kitu kikienda sawa, tutayafanyia Dar es Salaam, na kipindi chote hiki cha mapumziko ya FIFA, sisi tutakuwa kambini," Matei alisema.
Matei alisema sababu kubwa ya kuweka kambi Dar es Salaam ni kuwa karibu na eneo ambalo mchezo wao dhidi ya JKT Tanzania utachezwa.
"Mchezo wetu wa kwanza baada ya mapumziko hayo ni dhidi ya JKT Tanzania uatakaochezwa Dar es Salaam, na hiyo ndiyo sababu kubwa imesababisha tuwe huko karibu zaidi au sehemu hiyo hiyo ambayo tutacheza mchezo wetu wa Novemba 24," Matei aliongeza.
Prisons iliyoko chini ya Kocha Mkuu, Mbwana Makata, ipo katika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 10 kibindoni baada ya kucheza michezo 10, imeshinda miwili, sare nne na kupoteza mechi nne.
Kikosi cha JKT Tanzania nacho kinaendelea na mazoezi huku uongozi ukisema wachezaji wote walioumia katika ajali wanaendelea vyema na wameanza mazoezi mepesi chini ya uangalizi wa madaktari wa timu hiyo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED