BAADA ya Pacome Zouzoua kurejea kikosini kwa kupona kwa asilimia 100, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, ameahidi kufanya mabadiliko makubwa katika kikosi chake kuelekea katika mechi ya marudiano ya robo fainali, Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns Ijumaa wiki hii.
'Jeshi' lote la kikosi cha Yanga, akiwemo nyota huyo liliondoka nchini jana na kutua Afrika Kusini salama huku likipata mapokezi mazuri kutoka kwa Balozi wa Tanzania nchini humo, James Bwana.
Katika mchezo huo wa mkondo wa pili utakaochezwa Uwanja wa Loftus Versfeld, Pretoria, Yanga inahitaji ushindi wowote ili kutinga nusu fainali baada ya mchezo wa kwanza Uwanja wa Benjamin Mkaba, Dar es Salaam kutoka suluhu.
Yanga iliwakosa Pacome, Khalid Aucho na Yao Attohoula katika mchezo huo wa kwanza kutokana na kuendelea kuuguza majeraha yao, lakini wachezaji hao wote wameongozana na timu na Gamondi ana uhakika zaidi wa kumtumia Pacome.
Akizungumza na Nipashe jana kabla ya timu hiyo kuondoka nchini, Gamondi alisema ana matumaini mkubwa ya kufanya vizuri katika mchezo huo wa marudiano dhidi ya Mamelodi Sundowns.
Alisema hautakuwa mchezo rahisi kwa sababu mpinzani wake anafaida ya kucheza nyumbani lakini anaingia katika mchezo huo kwa kuziba njia zote ambazo wapinzani wao wanaweza kupata ushindi.
“Ni kweli Pacome amerejea kikosini na yupo fiti ninamatarajio makubwa ya kufanya mabadiliko ya kikosi katika mchezo wetu wa marudiano, wachezaji wanatakiwa kumwaga jasho ili kupata matokeo mazuri.
"Ukiwa na timu nzuri huwezi kuhofia mpinzani, malengo yetu makubwa ni kushinda mataji yote na kufanya vizuri zaidi, tunajua tunaenda kucheza na timu ya aina gani, licha ya kuzuia pia tunahitaji kushambulia,” alisema Gamondi.
Aliongeza kuwa Mamelodi Sundowns ni wazuri, lakini amejipanga kukabiliana nao katika mchezo huo wa ugenini kuhakikisha wanafanikiwa kupata ushindi ugenini jambo ambalo kwenye mpira linawezekana.
Gamondi alisema kazi kubwa anayoifanya kwa siku chache ni kuwajenga kisaikolojia wachezaji wake kutocheza kwa presha hasa safu ya ulinzi na ushambuliaji kuwa makini.
Katika hatua nyingine, Yanga ilieleza kupata mapokezi mazuri kutoka kwa Balozi wa Tanzania nchini Misri, James Bwana, baada ya kuwasili jana mchana.
Jana Serikali kupitia Naibu Waziri wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma maarufu Mwana FA, alisema imezitaka balozi zake nchini Afrika Kusini na Misri kuhakikisha zinahakikisha usalama unapatikana kwa Yanga na Simba zikiwa Afrika Kusini na Misri.
Simba nayo imeondoka leo alfajiri kuelekea Misri tayari kwa mchezo wao wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ambao nao utachezwa Ijumaa wiki hii.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED