Namungo yatamba kuipa kichapo Simba Jumatatu

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 07:37 AM Apr 26 2024
Kocha Mkuu wa Namungo, Mwinyi Zahera.
Picha: Mtandaoni
Kocha Mkuu wa Namungo, Mwinyi Zahera.

BENCHI la ufundi la Namungo FC limesema linaendelea kuimarisha safu yake ya ushambuliaji kwa ajili ya kuhakikisha haipotezi mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba utakaochezwa Aprili 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani, Lindi.

Akizungumza na Nipashe jana, Kocha Mkuu wa Namungo, Mwinyi Zahera, alisema lengo la kuboresha idara ya ushambuliaji ni kuhakikisha wachezaji wake wanatumia vyema nafasi wanazopata na hatimaye kuzibakisha pointi tatu nyumbani.

Zahera alisema wataingia katika mechi hiyo kwa tahadhari kwa sababu wanaamini Simba pia itahitaji kupata ushindi na kuendelea kujiimarisha katika msimamo wa ligi hiyo.

"Kwa sasa nashughulika na safu ya ushambuliaji ili nipate matokeo mazuri katika mchezo dhidi ya Simba, mchezo huo unatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa," alisema Zahera. 

Kocha huyo aliongeza kwake kila mchezo ni muhimu kwa sababu anahitaji kumaliza msimu katika nafasi za juu lakini pia kuwapa furaha mashabiki wao.

"Tunaupa umuhimu mkubwa mchezo huo kwa sababu tunafahamu tunakutana na timu ambayo imetoka kushiriki mashindano ya kimataifa, vile vile ina wachezaji wengi wa kimataifa wenye uzoefu," Zahera alisema.

Aliongeza mchezo huo utakuwa ni mwendelezo wa maandalizi ya mechi ya hatua ya robo fainali ya mashindano ya Kombe la FA dhidi ya Azam FC utakaopigwa ifikapo Mei 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam. 

Alisema pia wachezaji wote wanaendelea vyema isipokuwa mchezaji wake mmoja Fabrice Ngoma ambaye amevunjika mguu. 

"Fabrice amevunjika mguu kwa mujibu wa Daktari wetu hawezi kuonekana uwanjani mpaka msimu ujao kutokana na hali yake  ilivyo, " aliongeza Zahera.

Naye Katibu Mkuu wa timu hiyo, Ally Mkadeba, alisema mikakati yao ni kupata pointi tatu na uwezo wa kufanya hivyo wanao.

"Tuna matumaini makubwa ya kumfunga Simba, tuko kamili kila idara kuwakabili, tumejipanga vyema kuhakikisha tunafikia malengo," alisema Mkadeba.