Wakunga waja na maombi saba kwa serikali, UNFPA nao wana jambo lao

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 04:06 PM May 06 2024
Naibu Mwaklishi Mkazi UNFPA Tanzania, Melissa McNeil Barrett, wa pili kushoto na wadau wengine wakipiga makofi katika maadhimisho hayo.
Picha: UNFPA
Naibu Mwaklishi Mkazi UNFPA Tanzania, Melissa McNeil Barrett, wa pili kushoto na wadau wengine wakipiga makofi katika maadhimisho hayo.

CHAMA cha Wakunga Tanzania (TAMA), kimeiomba serikali kutekeleza mambo saba ambayo kinaona bado ni kikwazo kwa wakunga katika kutekeza majukumu yao ya kila siku kwa ufanisi.

Ombi la kwanza ni serikali kutengeneza mfumo wa kuwezesha wakunga kuhudumia akina mama na watoto wachanga wakati wa maafa, wakunga kujengewa uelewa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, athari zake kwenye afya ya uzazi, jinsi ya kuwahudumia waathirika na kuzuia matatizo yatokanayo na athari hizo.

Rais wa TAMA, Dk.Beatrice Mwilike ametoa maombi hayo katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani jijini Dar es Salaam ambayo yameratibiwa na TAMA kwa kushirikiana na shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) Tanzania.

"Tunaomba serikali kutengeneza Idadi ya wakunga katika vituo vya kutolea huduma kwa kutoa ajira mahususi kwa wakunga wanaomaloza mafunzo na kuhitimu ambao bado hawajaajiriwa," amesema Dk.Beatrice.

Ametaja ombi la nne kuwa kutaka mazingira ya kutolea huduma kwa wakunga yaboreshwe zaidi, kuwajengea nyumba karibu na vituo vya kutolea huduma, Kwa kuwa huduma zao zinahitaji saa 24, na kwamba wakati mwingine ni za dharura.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mara baada ya kuwakabidhi vyetu wakunga waliosaidia akina mama katika mafuriko ya Hanang mkoani Manyara na Rufiji mkoani Pwani. Kulia ni mwakilishi wa Balozi wa Canada nchni, Hellen Fytche, Rais wa TAMA, Dk. Beatrice Mwilike na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu (kushoto).

Rais huyo amesema, wakunga wanaomba kuanzishwa kwa mafunzo ya ualimu wa ukunga ili wahitimu wa ukunga wanaomaliza mafunzo, watoke na ujuzi na stadi za kutosha.

"Tunaomba kutambuliwa kwa taaluma ya ukunga katika mfumo wa utumishi umma, kwani wakunga wakihitimu, bado wanaajiriwa kwa cheo Ofisa Muuguzi kitendo ambacho  kinasababisha kupunguza morali ya kufanya kazi," amesema.

Katika ombi lao la saba, wanatamani walipwe mishahara na marupurupu mengine kulingana na ngazi zao za elimu, hasa kuanzia ngazi ya wakunga wabobezi.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, amewaagiza  watumishi wa Wizara ya Afya, wadau wa afya na jamii kushirikiana ili kuboresha huduma ya afya ya mama.

 Amesema,  watumishi wa wizara ya afya washirikiane na vyama vya kitaaluma kama Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA), kwa kuwa wadau muhimu katika afya.

 "Huduma ukunga zinahitaji ushirikiano kati ya wadau wa afya na jamii kwa ujumla kwa kuzingatia kuwa kila aliyezaliwa amepitia mkononi mwa wakunga," amesema Majaliwa.

 Amesema, njia hiyo itasaidua kuendelea kupunguza idadi ya vifo vya mama wajawazito na watoto vinavyotokea wakati wa kujifungua.

"Ushirikiano huo na wadau umesaidia kupunguza vifo hivyo  kutoka 558 mwaka 2015/16 hadi kufikia 104  mwaka 2022, hiyo ni hatua nzuri," amesema.

 Naibu Mwaklishi Mkazi UNFPA Tanzania, Melissa McNeil Barrett, amesema, kwa kutambua umuhimu wa mkunga, shirika hilo limezindua mradi uitwao kuwezesha mradi wa 'Thamini uzazi salama project'.

 Amesema mradi huo wa miaka saba, wenye thamani ya Dola milioni 12 za Kimarekani zilizotolewa na serikali ya Canada, utatekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam na Shinyanga kwa kujengea uelewa wakunga ili wafanye kazi yao kwa umakini zaidi.

 "Tutashirikiana na wadau mbalimbali ikiwamo serikali ya Tanzania, Canada, TAMA na wengine katika kutekeleza mradi huu kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Shinyana," amesema Melissa.