Lissu akabidhiwa gari baada ya miaka saba

By Peter Mkwavila , Nipashe
Published at 08:31 AM May 18 2024
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu akiwaonyesha waandishi wa habari na wanachama wa chama hicho, matundu ya risasi kwenye gari lake, baada ya kukabidhiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Dodoma jana.
Picha: Peter Mkwavila
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu akiwaonyesha waandishi wa habari na wanachama wa chama hicho, matundu ya risasi kwenye gari lake, baada ya kukabidhiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Dodoma jana.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amekabidhiwa rasmi gari lake ikiwa ni miaka saba tangu ashambuliwe kwa risasi na watu wasiojulikana huku akitamani kulipeleka Makumbusho ya Taifa.

Gari hilo, aina ya Toyota Landcruiser V8 VXR, lilikuwa limehifadhiwa kwenye Kituo Kikuu cha Polisi cha Dodoma tangu Septemba 7, 2017 lilipotokea tukio hilo nyumbani kwake, Area D jijini hapa. 

Akizungumza jana baada ya kukabidhiwa gari hilo na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Daniel Bendarugaho, mwanasiasa huyo alisema kama ingekuwa mapenzi yake, angetamani liwekwe makumbusho jinsi lilivyo bila kufanyiwa matengenezo lakini anahitaji usafiri kwa kuwa anatumia magari ya kuazima.

“Lakini nahitaji usafiri na magari ya kuazima azima pamoja na wema wa wanaowaazima sitaki kuwachosha sana, hivyo tutatengeneza ili ifanye kazi. Nitapendekeza liwekwe kwenye makumbusho ya nchi lakini kama wakubwa watasema hawataki kukaa na ushahidi wa namna hii tutatengeneza utaratibu wa kuhifadhi katika makumbusho binafsi,” alisema.

 Lissu aliwashukuru wanachama wa chama hicho kwa misaada na kuwa pamoja naye kwa kipindi chote tangu kutokea tukio hilo.

 Alisema katika risasi zilizopigwa kwenye gari hilo ziliingia maeneo mbalimbali ya mwili na kwamba hadi sasa bado anatembea na risasi mgongoni.

 “Mungu ni mwema bado nipo hapa, sasa hili gari tunachukua tukatengeneze tubadili milango, tutalihifadhi mahali gari lilikuwa jipya. Hili  halijaharibika sana linahitaji kutengenezwa ili lifanye kazi. Tuna kazi kubwa ya kufanya kama mnavyofahamu.

 “Litafanyiwa matengenezo lirudi kazini na siku ikifika haiwezi kufanya kazi basi tutarudishia hii milango tutafanya utaratibu iwekwe kwenye makumbusho ili watakaokuja baada yetu waje wajue kuna tukio baya liliwahi kutokea,”alisema.

 Lissu aliwaomba watu wema waliomsaidia wakati wa matibabu, wamsaidie kutengeneza gari hilo ili lifanye kazi.

 “Vilevile baadae nitaomba msaada utakapofika wakati wa kupelekwa kwenye makumbusho likawe somo kwa watoto wetu na wao watakaokuja baada ya sisi,”alisema.

Lissu alishukuru Jeshi la Polisi kwa kutunza gari hilo licha ya kuwa na eneo dogo la kuhifadhi vielelezo vya uhalifu.