VILIO, simanzi vyatawala jana wakati mwili wa Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dk. Faustine Ndugulile, ulipowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa, Julius Nyerere (JNIA).
Dk. Ndugulile alifariki dunia Jumatano wiki hii wakati akipatiwa matibabu nchini India.
Naibu Spika wa Bunge, Musa Azan Zungu, aliongoza viongozi mbalimbali waliojitokeza uwanjani hapo kuupokea mwili huo.
Viongozi wengine waliojitokeza ni mawaziri, wabunge, wakuu wa wilaya na watumishi wa Ofisi ya Bunge ambao waliungana na familia ya marehemu, kuupokea mwili huo, ambao ulipelekwa moja kwa moja Hospitali Kuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Lugalo.
Akizungumza na waandishi wa habari uwanjani hapo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, alimwelezea Dk. Ndugulile kama kiongozi aliyesimamia kile alichokiamini, hasa kikiwa kina maslahi ya wengi.
“Kama nchi tumepoteza mtu muhimu katika wakati muhimu. Alikuwa mtaaluma mzalendo, asiyebabaika na mazingira na mawimbi. “Nafasi ambayo aliipata WHO ilikuwa inakwenda kutusaidia na kunufaika kwa kuzaliwa kwake Tanzania. Ni huzuni kubwa,” alisema.
Simbachawene alisema alimfahamu Dk. Ndugulile tangu mwaka 2010 alipochaguliwa kwa mara ya kwanza na wananchi wa Kigamboni kuwa mbunge.
Mbunge wa Viti Maalum, Halima Mdee, alisema Dk. Ndugulile alikuwa ni mbunge wa aina yake, aliyetetea maslahi ya wananchi bila kujali itikadi za vyama.
Alisema ni kiongozi ambaye alikuwa mwerevu asiye na majivuno, ambaye aliwahi kushika shilingi bungeni, kutetea maslahi ya wananchi.
“Aliaminiwa na taifa, akasogezwa mbele kuwania nafasi hiyo ya kimataifa. Kwa hakika, nchi imepata pigo kubwa kwa kifo chake,” alisema.
Baadhi ya viongozi walioambatana na familia kuupokea mwili huo, ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi, wabunge wa Dar es Salaam, wakuu wa wilaya za Kigamboni na Temeke na baadhi ya wakazi wa jimbo la Kigamboni.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa juzi na Ofisi ya Bunge, kesho kutwa (Jumatatu) mwili utatolewa Lugalo na kupelekwa Parokia ya Mtakatifu Immaculata, Upanga, Dar es Salaam, kwa ajili ya ibada na kisha utapelekwa viwanja vya Karimjee kwa ajili ya mazishi ya kitaifa, yatakayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Baada ya Karimjee, mwili utalala nyumbani kwake Kigamboni na kesho yake, utapelekwa viwanja vya Machava, Kigamboni kwa ajili ya wananchi wake kumuaga na baadaye utazikwa katika makaburi ya Mwongozo, yaliyoko Kata ya Mwongozo, wilayani Kigamboni.
Dk. Ndugulile aliyezaliwa Machi 31, 1969, alifariki dunia Novemba 27, mwaka huu, akiwa nchini India alikokwenda kutibiwa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED