Waajiri wahimizwa kuimarisha utu na umakini kazini kuongeza ufanisi na ubunifu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:34 PM Nov 30 2024

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.
Picha:Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amewahimiza waajiri nchini kuongeza umakini na kuzingatia misingi ya utu mahali pa kazi ili iwe motisha na chachu kwa watumishi kuongeza ubunifu na ufanisi kazini.

Dk. Biteko amesema hayo wakati akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Phillip Mpango katika usiku wa Tuzo kwa mwajiri Bora wa mwaka 2024 ambapo Kampuni ya bia nchini (TBL) imeibuka mshindi wa jumla ikifuatiwa Kampuni ya Barick Gold huku Mamlaka ya Bandari Tanzania TPA ikishika nafasi ya tatu. 

Amewapongeza waandaaji wa tuzo hizo na kuwataka kupanua wigo wa makundi ya ushiriki huku akisisitiza umuhimu wa utoaji wa motisha mahala pa kazi ili watumishi waongeze ari ya kufanya kazi kwa viwango na ubora wajuu. 

“ Mwajiri anachokihitaji kwa mwajiriwa ni muda na ujuzi wake basi. Hivyo, waajiri ongezeni umakini na utu mahali pa kazi na mkifanya hivyo, waajiriwa ambao wanatumia muda mwingi kazini, wataongeza ubunifu na ufanisi na kuleta tija ya kazi,” amesema Dk. Biteko
                                                                     
Aidha, Dk. Biteko ameongeza kuwa Serikali inatambua mchango wa ATE katika maendeleo na program mbalimbali za maendeleo ikiwemo suala la ukuzaji wa uwiano wa kijinsia mahali pa kazi.

Akimkaribisha mgeni rasmi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na wenye ulemavu, Mhe. Ridhiwan Kikwete amesema Serikali kwa kushirikiana na Chama cha waajiri Tanzania (ATE) na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini TUCTA imeongeza makundi ya ushiriki kwa waajiri ikiwemo kigezo cha utambuzi wa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi pamoja na mwajiri anaezingatia masuala ya usawa wa kijinsia katika uajiri.

Ameongeza kuwa kwa msingi huo, Tanzania inajitanabaisha kimataifa kwa kuwa na Kiongozi Mkuu mwanamke (Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan) suala ambalo amesema linaiweka nchi katika nafasi ya juu kimataifa katika masuala ya usawa wa kijinsia.

Naye Mtendaji Mkuu wa ATE, Suzan Ndomba amesema tangu kuasisiwa kwa tuzo za mwajiri bora wa mwaka miaka 19 iliyopita washiriki wamekuwa wakiongezeka na kuongeza ufanisi na waajiri kuboresha mazingira ya kazi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Kanda ya Afrika Mashariki, Caroline Mugalla amepongeza hatua iliyofikiwa katika utoaji wa tuzo hizo, ameshauri mashindano hayo pia yahusishe na kutambua shughuli za vijana katika sekta isiyo rasmi ambayo ina mchango mkubwa katika jamii.

“Ni muhimu kuangalia namna ya kutambua mchango wa sekta isiyo rasmi ili kuweza kupata ajira zenye staha, amesema Mugalla. 

CHAMA CHA WAAJIRI TANZANIA (ATE):

Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) ni mojawapo ya vyama vya zamani nchini, kikiwa na historia ndefu ya kutetea maslahi ya waajiri na kuboresha mazingira ya kazi na biashara. Kiliundwa mwaka 1955 chini ya Trade Unions Ordinance na Societies Ordinance ya mwaka 1954 kwa jina la Dar es Salaam Association of Employers. Tangu wakati huo, chama kimepitia mabadiliko mbalimbali ya majina, hadi kufikia mwaka 1978 kilipoitwa rasmi Association of Tanzania Employers (ATE), kuondoa neno Tanganyika.

Kwa zaidi ya nusu karne, ATE imekuwa mshirika muhimu wa waajiri nchini, ikijitahidi kuboresha mazingira ya kazi kupitia utetezi, mafunzo, na ushauri wa kisheria. Hadi sasa, chama hiki kinajivunia wanachama waliodumu tangu miaka ya 1970, ambao wanatambuliwa kwa mchango wao katika kuimarisha utendaji wa ATE.

Tuzo ya Mwajiri Bora ya ATE (EYA 2024)

ATE imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha ushindani wa kibiashara kupitia Tuzo ya Mwajiri Bora (Employer of the Year Award - EYA). Tuzo hii, inayoratibiwa kila mwaka, inalenga kutambua kampuni na taasisi zinazofanya juhudi kubwa kuboresha mazingira ya kazi, ufanisi wa biashara, na ustawi wa wafanyakazi.

Mchakato wa tuzo hizi umeongeza hamasa na ushindani miongoni mwa waajiri, huku ukiimarisha viwango vya ufuataji wa sheria za kazi na utekelezaji wa sera bora zinazolenga tija. Mafanikio haya yanathibitisha dhamira ya ATE ya kushirikiana na waajiri kwa karibu ili kuendeleza maendeleo endelevu katika sekta ya kazi.

Ushirikiano na Serikali

ATE inatambua juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini. Kupitia mfumo wa majadiliano wa utatu unaojumuisha Serikali, waajiri, na wafanyakazi, ATE imekuwa mstari wa mbele kushughulikia changamoto mbalimbali zinazokabili sekta ya kazi na ajira.

Kwa niaba ya Bodi ya ATE, chama kimeahidi kuendelea kuboresha na kuratibu Tuzo ya Mwajiri Bora, pamoja na kuimarisha ushirikiano na Serikali ili kuhakikisha mazingira bora ya biashara yanaendelezwa.

Shukrani na Dira ya Baadaye

Mwenyekiti wa Bodi ya ATE, Oscar Mgaya, ametoa shukrani kwa wanachama, sekretarieti, na Serikali kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha malengo ya chama. Kwa miaka ijayo, ATE itaendelea kutetea maslahi ya waajiri, kubuni mipango bunifu, na kuimarisha ushindani wa kibiashara kwa maendeleo ya taifa.

ATE ni kiungo muhimu katika kuboresha uchumi wa Tanzania, kupitia usimamizi bora wa rasilimali watu na mazingira mazuri ya kazi.

6