WAZIRI wa Ujenzi Innocent Bashungwa,amefanya ziara Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga,kukagua ujenzi wa madaraja pamoja na kuzungumza na wananchi wa Bugomba kwenye mkutano wa hadhara.
Ziara hiyo imefanyika leo, Novemba 30, 2024, ikiongozwa na Waziri Bashungwa, pamoja na viongozi wa serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha.
Bashungwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan kupitia mfuko maalum wa kurudisha miundombinu iliyoathiriwa na mvua za El Niño na kimbunga Hidaya, ametenga kiasi cha shilingi bilioni 868 kwa nchi nzima kukarabati barabara na madaraja korofi. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 18.5 zimetolewa kwa Halmashauri ya Ushetu kwa ajili ya kukarabati madaraja manne yaliyoharibiwa na mvua, likiwemo daraja linalounganisha Ushetu na Geita.
“Halmashauri hii inatekeleza miradi ya ujenzi wa madaraja matatu yenye thamani ya shilingi bilioni 13.5, na kuna daraja la nne lenye thamani ya bilioni 5 linalojengwa ili kuunganisha Ushetu na Geita. Miradi hii yote itagharimu jumla ya shilingi bilioni 18.5,” amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa amemwagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Samweli Mwambungu, kuhakikisha wakandarasi wanasimamia miradi hiyo kwa weledi ili thamani ya fedha ionekane, na kuanza ujenzi wa daraja linalounganisha Ushetu na Geita mara moja. Alisisitiza kwamba miradi yote inapaswa kukamilika ndani ya mwaka mmoja.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, amepongeza jitihada za Rais Samia kwa kutatua changamoto za miundombinu, akibainisha kuwa wakazi wa Ushetu, ambao wengi ni wakulima wa tumbaku, walikuwa wakikumbwa na changamoto kubwa kutokana na uharibifu wa madaraja hayo.
Mbunge wa Ushetu, Emmanuel Cherehani, amesema kwamba ujenzi wa madaraja haya utaondoa kero za muda mrefu kwa wananchi wa jimbo lake, huku Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, akieleza kuwa serikali imewatendea haki wananchi wa Ushetu kupitia miradi hiyo.
Awali, Meneja wa TANROADS Shinyanga, Mhandisi Mwambungu, alifafanua kuwa madaraja yanayojengwa ni Ubagwe (bilioni 4.1), Kasenga (bilioni 5.1), na Ng’wande (bilioni 4.1). Aliongeza kuwa ujenzi wa daraja la Ubagwe unatekelezwa na Kampuni ya Salum Motor Transport Limited kwa muda wa miezi 12.
Wananchi wa Ushetu wameipongeza serikali kwa mradi huo, wakieleza kuwa madaraja hayo yatakuwa msaada mkubwa kwao, hasa katika shughuli za kiuchumi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED