USHINDI wa Azam FC wa mabao 2-1 ilioupata juzi dhidi ya Singida Black Stars kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara imeifanya kuondoka na pointi tatu katika michezo sita mfululizo, huku Kocha Mkuu wa timu hiyo, Rachid Taoussi akisema kwa sasa timu yake ni imara.
Tangu ilipolazimishwa suluhu dhidi ya Mashujaa FC kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Septemba 29 mwaka huu, Azam ikaanza kupata ushindi mfululizo hadi kufikia michezo sita kwa kuifunga Namungo bao 1-0, ikaishindilia Prisons mabao 2-0, ikaipa kipigo cha mabao 4-1, KenGold, kabla ya kuichapa Yanga bao 1-0, baada ya hapo ikaifunga Kagera Sugar bao 1-0, kabla ya juzi kushinda mabao 2-1, mechi ikichezwa, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Katika michezo hiyo, dhidi ya Namungo, Prisons na Yanga ilicheza ugenini, huku dhidi ya KenGold, Kagera Sugar na Singida Black Stars ikiwa nyumbani.
Azam imecheza michezo saba bila kupoteza, ambapo mara ya mwisho ilifungwa mabao 2-0 dhidi ya Simba, Septemba 26 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, baada ya hapo ikatoka suluhu dhidi ya Mashujaa FC na kuanza kushinda mfululizo.
Yalikuwa ni mabao ya Feisal Salum dakika ya 38 na Jhonier Blanco dakika ya 57 yaliyotosha kuwapa ushindi huo, huku Elvis Rupia akiifungia Singida bao la kufutia machozi dakika ya 62.
Kocha Mkuu wa Azam, Taoussi, alisema timu yake kwa sasa imeimarika kwa kutosha, lakini pia aliwatahadharisha wachezaji wake kuwa makini kwani walikuwa wanacheza na moja kati ya timu bora kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
"Nina furaha sana mimi, wachezaji na mashabiki wetu, kwa sasa Azam imekuwa timu imara, kwani tumeishinda timu nzuri ya Singida Black Stars, niliwaambia wachezaji wangu wawe makini kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchezo, nashukuru tunasonga mbele," alisema kocha huyo.
Ramadhani Nsanzurwimo, Mkurugenzi wa Ufundi wa timu hiyo, ambaye ameachiwa mikoba ya kuifundisha timu hiyo kwa muda baada ya kutimuliwa kwa Patrick Aussems na msaidizi wake Denis Kitambi, amesema wachezaji wake wameonekana kuathirika na tukio hilo.
"Wachezaji wangu walichelewa sana kuingia kwenye mchezo, nadhani mabadiliko ya makocha yameonekana kuwaathiri, bado akili zao ni kama haziamini au hawajakubaliana na hali, lakini kipindi cha pili tulirudi mchezoni na kuwashambulia wapinzani wetu, hii inanipa matumaini kuwa tutafanya vyema mchezo ujao," alisema.
Ushindi huo, umeipandisha Azam hadi nafasi ya pili ya msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi 27 nyuma ya vinara Simba yenye pointi 28, huku Singida ikisalia nafasi ya nne na pointi zake 24.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED