Kilichomnasua Nawanda kesi ya ulawiti, mwenyewe asema anamwachia Mungu

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 10:00 AM Nov 30 2024
Kilichomnasua Nawanda kesi ya ulawiti, mwenyewe asema anamwachia Mungu.

"MUNGU ni mwema na kila kitu kinatoka kwa Mungu. Utukufu ni wake Mungu, yote ninamwachi Mungu." Hiyo ni kauli ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Yahaya Nawanda nje ya mahakama, muda mfupi baada ya kuachiliwa huru jana katika kesi ya mashtaka ya kulawiti mwanafunzi wa chuo kikuu.

Dk. Nawanda alikuwa anakabiliwa na kesi ya jinai namba 1883 ya mwaka 2024 katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Mkoa wa Mwanza.

Akisoma hukumu hiyo jana Hakimu Mfawidhi Mkuu, Erick Marley alisema mahakama hiyo ilipokea mashahidi 10 na vielelezo vitatu kutoka upande wa Jamhuri pamoja na shahidi mmoja kutoka upande wa utetezi ambaye ndiye alikuwa mshtakiwa katika kesi hiyo.

Hakimu huyo alisema kuwa kati ya mashahidi wa upande wa Jamhuri, mama mzazi wa binti aliyedaiwa kuingiliwa kinyume cha maumbile, alikuwa shahidi namba moja, shahidi namba mbili ni binti mwenyewe. Wengine ni askari wa upelelezi, uchunguzi, daktari kutoka Hospitali ya Rufani Mkoa wa Mwanza (Sekou Toure) na mtaalamu wa Tehama kutoka Jengo la Rock City Mall.

Alisema vielelezo vilivyowasilisishwa mahakamani huko ni pamoja na picha mjongeo (CCTV footage) za eneo la jengo hilo, gari ambako tukio lilidaiwa kutokea, vipimo vya daktari pamoja na maelezo ya awali aliyoandikisha binti huyo.

Hakimu Marley alisema mahakama ilimkuta Dk. Nawanda na kesi ya kujibu, hivyo kumpa nafasi ya kujitetea na baada ya kujiridhisha kutokana na ushahidi uliotolewa na pande zote mbili, hakutiwa hatiani.

Alitaja mambo yaliyotia shaka katika vielelezo na ushahidi uliotolewa na mashahidi hao ni pamoja na kukosekana baadhi ya vipande vya video (CCTV footage) zinazoonesha binti huyo akifanyiwa ukatili kati ya vilivyowasilishwa mahakamani.

Alisema video hizo zinamwonesha binti huyo wakati akiingia katika geti akiwa amepakizwa kwenye pikipiki, akaanza kufanya mawasiliano kisha nyingine zilionesha wakati mshtakiwa Dk. Nawanda aliposhuka kulipia ushuru wa maegesho.

Hakimu huyo alisema hakuna video zilizomwonesha binti huyo akiingia katika gari na chochote kilichoendelea ndani ya gari hilo, hivyo kutothibitisha juu ya kutendeka ukatili huo.

Vilevile, hakimu huyo alisema mahakama haikupokea ushahidi wa vinasaba (DNA) unaonesha kuwa aliyemwingilia kinyume cha maumbile ni nani licha ya binti huyo pamoja na mshtakiwa kuchukuliwa vipimo hivyo, hali iliyofanya mahakama hiyo kukosa ushahidi wa kitaalamu juu ya tukio hilo.

Hakimu Marley alisema licha ya daktari kuthibitisha kuwa binti hiyo aliingiliwa kinyume cha maumbile kutokana na sehemu zake za siri kuwa na michubuko kwa ndani na nje, ushahidi huo haukubainisha nani aliyemwingilia.

"Katika ushahidi uliotolewa na Daktari Patrick Daudi kutoka Hospitali ya Rufani Mkoa wa Mwanza (Sekou Toure), alisema binti huyo alifikishwa hospitalini huko kwa ajili ya vipimo baada ya saa zaidi ya 19 tangu alipotendwa tukio hilo huku akiwa tayari ameoga na kuondoa ushahidi wa mbegu za kiume, hivyo kukosa ushahidi wa mbegu ili kudhihirisha kuingiliwa kingono na mtu yupi," alisema Hakimu Marley.

Alisema kuchelewa kwa binti huyo kwenda hospitalini huku kukiwa na mtu mwingine aliyetajwa kuwa mwenzake waliokuwa wakiishi wote, viliweka shaka juu ya kama kuna mtu mwingine aliyemtenda tukio hilo kwa muda wote huo.

"Katika ushahidi wake, shahidi namba moja ambaye ni binti huyo alieleza kuwa baada ya kutendwa tukio hilo, alikwenda moja kwa moja alikokuwa anaishi na kisha kumweleza rafiki yake kisha kuwasiliana na mama yake, lakini shahidi huyo hakumleta mahakamani hapa, pengine angekuwa shahidi muhimu," alisema Hakimu Marley.

Alisema sehemu nyingine iliyoacha shaka ni maelezo ya binti huyo aliyedaiwa kulawitiwa, kwamba alifanyiwa ukatili huo katika gari jeupe, lakini rangi yake halisi ni ya fedha.

Pia alisema binti huyo alidai kuwa wakati anafanyiwa kitendo hicho, gari lilikuwa na vioo 'tinted' na nje hakukuwa na watu waliokuwa wanapita, lakini video zilionesha gari hilo halikuwa 'tinted' na pia watu waliokuwa wakipita nje na kuendelea na shughuli zao.

Alisema kuwa baada ya Dk. Nawanda kukutwa na kesi ya kujibu, alipotakiwa kujitetea, alikiri kuwa siku hiyo ya tukio alifika katika eneo hilo kwa ajili ya kuchukua mahitaji yake na pia alikiri kuwasiliana na binti huyo kama rafiki yake na hawakutumia muda mrefu aliondoka kwa kuwa alikuwa na miadi na watu wengine.

Hakimu huyo alisema kama ilivyo kwa mujibu wa video za CCTV, aliingia eneo hilo saa 2:48 na kutoka saa 3:11 usiku, wakitumia dakika 23 pekee na kuwa yeye na binti huyo hawakuwahi kukutana katika gari na wala gari hilo halikuwa na vioo vyeusi (tinted) kama alivyodai binti huyo.

Baada ya kusikiliza pande zote, Hakimu Marley alimwachilia huru Dk. Nawanda na kueleza kuwa kutokana na kasoro hizo zilizojitokeza na baada ya kuhusianisha na kesi nyingine za namna hiyo, mahakama haikumkuta na hatia mshtakiwa huyo, hivyo yuko huru.

Baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo katika mahakama hiyo iliyokuwa imefurika watu, Nipashe ilishuhudia hisia tofauti vilio na kelele za shangwe.

Katika ufuatiliaji wake, mwandishi alibaini binti huyo aliyedai kutendwa ukatili huo, pia mama yake mzazi hawakuwapo wakati hukumu hiyo ikisomwa.

Akizungumza nje ya mahakama hiyo, Dk. Nawanda alisema anamshukuru Mungu kwa kila kitu pamoja na ndugu, jamaa na marafiki na mawakili waliosimama naye katika kipindi hicho chote.

"Ninaishukuru familia yangu, ninaishukuru mahakama imetenda haki, Wakili Alex kwa kazi kubwa aliyofanya, ninamshukuru Mungu kwa kila kitu. Mungu ni mwema na kila kitu kinatoka kwa Mungu na utukufu ni wake Mungu. Asenteni sana! Ninamwachia Mungu," alisema Dk. Nawanda.

Wakizungumza nje ya Kituo Jumuishi katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Mkoa wa Mwanza, mawakili wa upande wa utetezi, wakiongozwa na Costantine Mutalemwa, walisema mteja wao hana nia ya kufungua shauri la kuchafuliwa kisiasa kwa kuwa kila kitu mteja wao amemwachia Mungu.

Dk. Nawanda alipandishwa kizimbani kwa kwa mara ya kwanza Julai 9, 2024 na kusomewa shtaka moja la kumlawiti binti huyo, kitendo ambacho ni kinyume cha kifungu namba 154(1)(a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, SURA 16.

Alidaiwa kutenda tukio hilo Juni 2 mwaka huu, akidaiwa kumtenda ukatili huo mwanafunzi huyo wa chuo kikuu cha mkoani Mwanza katika eneo la maegesho ya magari lililoko Rock City Mall, wilayani Ilemela, mkoani Mwanza.