Yanga kurejesha furaha

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:16 AM Nov 30 2024
news
Picha:Yanga
Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic.

KOCHA Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic amesema wamejiandaa vyema kwa ajili ya mchezo wa leo, huku akisema wachezaji wake watapambana kwa kila hali kupata ushindi ili kurejesha furaha kwa wanachama na mashabiki wa timu hiyo.

Leo, Mabingwa Watetezi wa Ligi Kuu, Yanga watashuka kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa, Lindi kucheza dhidi ya Namungo, mchezo unaotarajiwa kuanza saa 12:30 jioni.

Yanga itaingia uwanjani leo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza michezo miwili ya Ligi Kuu, baada ya kufungwa bao 1-0 na Azam Novemba 2, mwaka huu na ikafungwa 3-1 na Tabora United, Novemba 7 mwaka huu, mechi zote zikichezwa, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Pia itaingia uwanjani ikitoka kupoteza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, baada ya kufungwa mabao 2-0 na Al Hilal ya Sudan, Jumanne iliyopita, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kocha Ramovic, amesema kila kitu kimekwenda vyema, ila wamejipanga kushinda mchezo wa leo ili kuwarudishia furaha Wanayanga.

"Maandalizi yamekamilika, hii ni mechi muhimu kwetu, kila kitu kinakwenda vizuri, ila nakiri utakuwa mchezo mgumu ila tumejipanga kuondoka na pointi zote tatu.

Hii itakuwa ni mechi yangu ya kwanza nikiwa na Yanga kwenye Ligi Kuu, na ya kwanza pia nikicheza ugenini, lakini haichezwi kwa ajili yangu, ila kwa ajili ya timu, najua tumepoteza michezo miwili mfululizo ya ligi, lakini hilo haliwezi kutufanya tusipambane na kupata ushindi," alisema kocha huyo.

Hata hivyo, alisema Yanga inawakosa wachezaji Shadrack Boka, Clement Mzize, huku pia kukiwa na hati hati ya kukosekana kwa kipa namba moja, Djigui Diarra.

"Diarra naye yuko kwenye hati hati, itategemea na hali yake itakavyokuwa, hivyo inawezekana akakaa langoni au la," alisema kocha huyo raia wa Ujerumani.

Naye Kocha Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda, amesema wataingia uwanjani kwa kuiheshimu Yanga, kwani pamoja na kupoteza mechi zake kwa siku za karibuni, lakini bado ni mabingwa watetezi.

"Ni mechi ambayo tunahitaji matokeo mazuri, tunakwenda kwa tahadhari kwani tunacheza na timu kubwa, itakuwa mechi ngumu kwa sababu wametoka kupoteza kwenye michezo yao iliyopita, lakini tumejiandaa kushinda mchezo.

"Kingine ni kwamba hatuendi kucheza na mwalimu mgeni, tunakwenda kucheza na Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, kwa hiyo tumejiandaa kucheza na timu siyo kocha mpya," alisema.

Yanga ipo nafasi ya tatu ya msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 24, kwa mechi 10 ilizocheza, huku Namungo ikikamata nafasi ya 13 ya msimamo, ikiwa na pointi tisa kwa michezo 11 iliyocheza.