Ahoua afichua siri ya penalti Simba

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:00 AM Nov 30 2024
KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Jean Charles Ahoua.
Picha:Mtandao
KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Jean Charles Ahoua.

KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Jean Charles Ahoua, amefichua kuwa yeye ndiye mpigaji penalti namba moja kwenye kikosi hicho ambapo ameshaaminiwa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids na wachezaji wenzake.

Ahoua ambaye ni raia wa Ivory Coast aliyesajiliwa na Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea klabu ya Stella Club d’Adjame ya nchini humo, Jumatano iliyopita alifunga bao kwa mkwaju wa penalti katika mchezo wa kwanza wa makundi wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravo do Maquis ya Angola na kuipatia timu hiyo ushindi wa bao 1-0.

Alisema kuwa katika muda mfupi tu ambao amekuja kwenye klabu ya Simba, tayari Kocha Fadlu na wachezaji wenzake wamemwamini kwenye upigaji penalti.

"Nashukuru kwa kocha na wenzangu kuniamini kuwa mpigaji penalti namba moja wa timu, wamekuwa na imani sana na mimi, nashukuru Mungu kwa hilo, pia sijawaangusha kwani zote ambazo nimepewa nimekuwa nikifunga na nitaendelea kufanya hivyo zikipatikana zingine kwa sababu najiamini na naamini kuwa naweza kufunga," alisema mchezaji huyo.

Kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, mchezaji huyo amefunga penalti zote mbili ambazo amepewa kupiga kati ya nne ambazo Simba imezipata.

Alipachika mkwaju wa penalti katika mchezo ambao timu hiyo ilicheza dhidi ya Dodoma Jiji na kuiwezesha kushinda bao 1-0, pia dhidi ya KMC, akiiongoza Simba kushinda mabao 4-0, huku mbili zingine ilizozipata zikipigwa na Leonel Ateba, naye pia akiweka zote kwenye kamba, kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union ilipotoka sare ya mabao 2-2, na dhidi ya Pamba iliposhinda bao 1-0.

Ahoua alikiri kuwa mchezo dhidi ya Bravo do Maquis ulikuwa mgumu, lakini anashukuru kupata ushindi ambao umepatikana kwa bao alilofunga.

Naye Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema wamefurahishwa na ushindi huo ambao umewapa pointi tatu, huku ikisema michuano hiyo inahitaji zaidi matokeo ya ushindi kuliko maonesho.

"Tumefurahi na ushindi tulioupata kwa kuiheshimisha nchi, hii ni michuano ya Afrika, tunachohitaji ni kukusanya pointi tatu kwa maana hiyo tumetimiza malengo, mashindano haya hayahitaji mbwembwe.

“Kuna wengine wanatubeza kuwa tumepata bao la penalti, lakini wakumbuke kuwa hata kufunga kwa penalti nako kunahitaji umahiri na ufundi, ndiyo maana Simba ilipata penalti yake Ahoua akafunga, wenzetu wakapata lakini kipa wetu Moussa Camara akaokoa, hii yote ni kuonesha tuna wachezaji wenye uwezo, ubora na vipaji, siyo kila penalti ikipatikana basi unaweza kufunga," alisema Ahmed.

Desemba 8, Simba itacheza saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Mohamed Hamlaoui dhidi ya CS Constantine ya Algeria katika mchezo wa Kundi A, Kombe la Shirikisho Afrika.