Pacha wafariki dunia nyumba ikiteketea moto

By Christina Haule , Nipashe
Published at 12:09 PM May 06 2024
Moto waunguza watoto pacha.
PICHA: MAKTABA
Moto waunguza watoto pacha.

WATOTO wawili pacha, Bright na Brown George Banzi, wenye umri wa miaka mitano, wamefariki dunia na ndugu yao mwingine kujeruhiwa baada ya nyumba walimokuwa wamelala kuteketea kwa moto unaodaiwa kutokana na hitilafu ya umeme.

Ofisa Habari Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Benjamin Bandula, amethibitisha watoto hao kufariki dunia na kumtaja aliyejeruhiwa kuwa ni Kulwa George Banzi, mwenye umri wa miaka tisa baada ya kujiokoa kwa kutoka nje ya nyumba hiyo.

Bandula, amesema tukio hilo lilitokea Jumamosi iliyopita majira ya saa mbili usiku Mtaa wa Kibao cha Shule Kata ya Kihonda, Manispaa ya Morogoro.

Amesema taarifa za tukio la nyumba hiyo kuungua, zililiripotiwa na Jeremia Majinja.

Amesema Majinga, ameliambia jeshi hilo kuwa nyumba hiyo yenye vyumba vinne inayomilikiwa na George Banzi, inateketea kwa moto na inadaiwa kuwa chanzo cha tukio hilo kwa mujibu wa mashuhuda inawezekana ni hitilafu ya umeme kwa kuwa ulikuwa unakatika na kurudi kila mara.

Amesema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo halisi cha tukio hilo na kuahidi kutoa taarifa baada ya kukamilika.

Vilevile Bandula, amesema wanaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini madhara na thamani ya mali zilizotokea ikiwa ni pamoja na nyumba hiyo na samani za ndani baada ya kuteketea kwa moto.

Awali, amesema nyuma hiyo imeteketea kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza ikiwamo jeshi hilo kuchelewa kupata taarifa za tukio hilo na ubovu wa miundombinu ya barabara uliosababisha gari lao kuchelewa kufika kwa wakati.

“Ni kweli kioo cha mbele cha gari kimepasuliwa, mashuhuda waliougundua moto ukiwa umeshika sehemu kubwa ya nyumba, wananchi wakati wakijaribu kuuzima wenyewe baadaye wakatoa taarifa kwetu wakati moto ulikuwa umeshasambaa kwenye nyumba yote,” amesema Bandula.

Wakazi wa eneo hilo walihamaki na kujaribu kushambulia gari la Zimamoto wakidai limechangia kuteketea kwa nyumba hiyo baada ya kuchelewa kufika katika eneo la tukio.

Tukio hilo limedhibitiwa na askari wa Jeshi la Polisi na viongozi wa serikali ya mtaa huo waliokuwa eneo la tukio baada ya kuwatuliza wakazi hao.