Waume wadaiwa kuwapiga wake zao na kuwapora mikopo

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 05:04 PM May 06 2024
Waume wadaiwa kupiga wake zao.
PICHA: MAKTABA
Waume wadaiwa kupiga wake zao.

BAADHI ya wajasiriamali wanawake wa Kata ya Mwamala wamedai hawanufaiki na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kutokana na kuambulia vipigo na kuporwa na waume zao na kushindwa kurejesha.

Wametoa madai hayo wakati wakizungumza na Nipashe kuhusu utekelezaji wa mradi wa wanajamii na vyombo vya habari katika kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto unaofadhiliwa na Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT).

Mwenyekiti wa Kikundi cha Vumilia,  Ester Mandi, amesema pamoja na  serikali kuwa na lengo la kuwainua kiuchumi kwa kupatia fedha mikopo isiyokuwa na riba ili kukuza mitaji yao,  wanapogawana kwa lengo la kuwekeza katika biashara, wananyang’anywa na waume zao na kushindwa kurejesha.

Amesema ili kudhibiti tatizo hilo ni vyema serikali iwaelimishe wanaume ili watambue mikopo inayotolewa kuwaendeleza wanawake na vijana.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Mkombozi,  Anna Nkinga, amesema walikopeshwa Sh.milioni 4 kwa ajili ya kuanzisha mradi wa ufugaji ngo’mbe, lakini wameingiliwa na waume zao kwa madai mwanamke hawezi kufanyabiashara wakati mwanaume yupo na kusimamia wao.

“Mkopo huu tumefanikiwa kuulipa wote na kikundi chetu hakidaiwi, lakini marejesho yake ilikuwa ni kuvutana mpaka Ofisa Maendeleo wa Jamii alipoingilia kati tena kwa kuwaita waume zetu kwa barua na kuwalazimisha kulipa," amesema Nkinga.

Ofisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Mwamala, Sophia Philbert amethibitisha  baadhi ya vikundi vya ujasiriamali vilivyopokea mikopo hiyo kushindwa kurejesha.

Hata hivyo, Sophia, amesema ofisi yake itahakikisha vikundi hivyo vinarejesha mikopo hiyo ili kuvipatia fursa vingine kunufaika na fedha hizo za serikali.

Amesema baadhi ya wanaume wamekuwa wakifika ofisini kwake kuilalamikia  serikali kwa kuwapatia mikopo hiyo wanawake na vijana na kuwaacha wao wakati wana uwezo wa kufanya biashara.

Amesema ofisi yake imebaini kuna wanaume wamebuni mbinu ya  kuwatumia wanawake kuunda vikundi, kuwakopea fedha na kuwakabidhi jambo ambalo ni kinyume na sheria.