Hama hama ya wafugaji yaachisha shule wanafunzi

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 05:39 PM May 06 2024
Watoto wakichunga ng'ombe.
PICHA: MAKTABA
Watoto wakichunga ng'ombe.

TABIA ya baadhi ya wafugaji wa Kijiji cha Ng’homango wilayani hapa kufuata malisho inadaiwa kusababisha wanafunzi kuacha shule na kushindwa kutimiza ndoto ya kupata elimu.

Hayo yamesemwa na Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Ng’homango, Peter Yuga wakati akizungumza na Nipashe shuleni hapo kuhusiana na tatizo hilo.

Yuga, amesema hali ya uhamaji kijijini hapo ni kubwa huku wanafunzi wakiachishwa  masomo bila kujali hata wale waliopo kwenye madarasa ya mtihani.

“Mwaka jana tulifanikiwa kumtafuta kwa ushirikiano na viongozi wa serikali na kumrejesha mwanafunzi wa darasa la nne ili afanye mitihani na kuendelea na masomo baada ya kutoroshwa,” amesema Yuga.

Ametoa wito kwa wazazi ambao ni wafugaji  wanapotaka kuhama kwenda kutafuta malisho mikoa mingine, waangalie uwezekano wa kuacha familia zao ili watoto waendelee na masomo hasa wa madarasa ya mtihani ili waweze kutimiza ndoto zao.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ng’homango, Madilya Nyema, amesema mwaka jana hali ilikuwa mbaya zaidi kutokana na wafugaji kuhamishwa katika eneo la Hifadhi ya Msitu wa Nindo.

Nyema, amesema serikali na  walimu wamekuwa wakishirikiana kudhibiti wanafunzi kuachishwa shule ili waendelee kupata elimu kwa kuwa ni haki yao ya msingi.