Mzava akemea unyanyapaa kwa watoto wenye uhitaji maalumu

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 03:21 PM May 06 2024
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Godfrey Mzava (Wa kwanza kulia) akizungumza na wa wanafunzi.
Picha: Julieth Mkireri.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Godfrey Mzava (Wa kwanza kulia) akizungumza na wa wanafunzi.

KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Godfrey Mzava amekemea tabia ya baadhi ya watu kwenye jamii kuwabagua na kuwanyanyasa watoto wenye mahitaji maalumu.

Mzava amesema mbali ya unyanyasaji pia wapo wanaoendelea kuwaficha watoto hao na kuwanyima haki zao za msingi.

Kiongozi huyo ameyasema hayo leo Mei 6, 2024 wakati Mwenge wa Uhuru ulipokimbizwa katika Wilaya ya Kibiti Mkoa wa Pwani. Amesema, jamii inatakiwa kuacha tabia ya kuwatenga watoto wenye ulemavu badala yake wawasimamie kupata haki zao.

Amesema serikali kwasasa inaendelea kuboresha mazingira wezeshi kwa watoto wenye mahitaji maalumu hivyo jamii nayo inatakiwa kuachana na tabia za kuwabagua.

"Nimeisikia hapa serikali imekuwa ikitoa sh. milioni 1.3 kila mwezi kwa ajili ya kupata chakula na mahitaji maalumu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, tuendelee kusimamia mahitaji yao muhimu," amesema.

Aidha amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa kundi hilo kwa kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya na huduma nyingine hivyo jamii nayo inatakiwa kuunga mkono juhudi hizo.

Kadhalika ameikumbuaha jamii kuzingatia uendelevu na utunzaji wa mazingira kama ambavyo Ofisi ya makamu wa Rais inavyoelekeza kupanda Milion 1.5 ili kurudisha uoto wa asili.

Amesema shughuli zote za uzalishaji ikiwa ni pamoja na viwanda lazima zizingatie uendelevu na utunzaji wa mazingira.

Awali akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka Wilaya ya Rufiji Mkuu ya Kibiti Kanal Joseph Kolombo amesema Mwenge huo utakimbizwa km 83.7 ambapo utaifikia miradi ya maendeleo 15 yenye thamani ya sh. biloni 2.4.