Kimbunga Hidaya kilivyoathiri watahiniwa kidato cha sita

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 12:34 PM May 06 2024
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk. Said Mohamed.
PICHA: MAKTABA
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk. Said Mohamed.

BARAZA la Taifa la Mitihani (NECTA) limetangaza kuanza kwa Mitihani ya Kidato cha Sita (ACSEE) na Ualimu ngazi ya Cheti na Stashahada, huku likieleza kuwa, mvua inayonyesha imeathiri shule moja mkoani Lindi ambayo watahiniwa wake watafanya mtihani huo kupitia kituo.

Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk. Said Mohamed, ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam wakati akitangaza kuanza kwa mitihani hiyo kuanzia leo hadi Mei 24, mwaka huu, kwa Kidato cha Sita na ya ualimu inatarajia kumalizika Mei 20, mwaka huu.

Dk. Mohamed amefafanua kuwa, shule ambazo inatarajia kufanya mtihani huo katika kituo ni Kilwa Sekondari kutokana na kuathiriwa na mvua inayoendelea kunyesha nchini.

“Kutokana na Kimbunga (Hidaya) tumepokea taarifa ya athari kwa  shule moja ya msingi ambayo hata hivyo, haiuhusiani na mihitani inayokwenda kuanza kesho (leo),” amesema.

Kuhusu mitihani hiyo, Dk. Mohamed amesema kwa Kidato cha Sita inafanyika katika jumla ya shule za sekondari 931 na vituo vya watahiniwa wa kujitegemea 258 na wa ualimu katika vyuo vya ualimu 99.

“Jumla ya watahiniwa 113,504 wamesajiliwa kuufanya mitihani ya Kidato cha Sita 2024 ambapo kati yao, watahiniwa wa shule ni 104,449 na wa kujitegemea ni 9,055,” amesema.

Amesema kati ya watahiniwa wa shule waliosajiliwa, wavulana ni 57,378 sawa na asilimia 54.9 na wasichana ni 47,071 sawa na asilimia 45.1.

Dk. Mohamed amesema watahiniwa wenye mahitaji maalum ni 232 ambapo kati yao, 201 ni wenye uoni hafifu , 16 ni wasioona na 15 ni wenye ulemavu wa viungo vya mwili.

Amesema kati ya watahiniwa wa kujitegemea 9,055 waliosajiliwa, wavulana ni 5,515 sawa na asilimia 60.91 na wasichana ni 3,540 sawa na asilimia 39.09. Watahiniwa wa kujitegemea wenye mahitaji maalum wako watatu ambao wote ni wenye uoni hafifu.

“Mwaka 2023 idadi ya watahiniwa wa shule na kujitegemea waliosajiliwa walikuwa 106,883, hivyo kuna ongezeko la jumla ya watahiniwa 6,621, sawa na asilimia 6.19 kwa mwaka 2024 ukilinganisha na mwaka 2023.

MTIHANI WALIMU

Dk. Mohamed amesema jumla ya watahiniwa 11,552 wamesajiliwa ambapo kati yao watahiniwa 2,766 ni wa ngazi ya Stashahada na watahiniwa 8,786 ni wa ngazi ya cheti.

Amesema ngazi ya stashahada, wanaume ni 1,634 sawa na asilimia 59.07 na wanawake ni 1,132 sawa na asilimia 40.93.

Amesema ngazi ya cheti, jumla ya watahiniwa 3,969 sawa na asilimia 45.17 ni wanaume na watahiniwa 4,817 sawa na asilimia 54.83 ni wanawake.

Amesema watahiniwa wenye mahitaji maalum waliosajiliwa ni 12 ambapo wenye uoni hafifu ni wawili kwa ngazi ya stashahada na wanane kwa ngazi ya cheti. Watahiniwa wasioona kwa ngazi ya cheti ni wawili.

Kwa mujibu wa Dk. Mohamed, mwaka jana idadi ya watahiniwa wa ualimu waliosajiliwa walikuwa 8,479, hivyo kuna ongezeko la jumla ya watahiniwa 3,073 sawa na asilimia 36.24 kwa mwaka 2024 ukilinganisha na mwaka 2023.

Katibu Mtendaji huyo amesema pamoja na maandalizi yote muhimu yaliyofanyika,  kamati za mitihani za mikoa na halmashauri zihakikishe usalama wa vituo unaimarishwa na kutumika kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa na baraza.

“Baraza linatoa wito kwa wasimamizi wote walioteuliwa kusimamia mitihani kufanya kazi yao kwa weledi na uadilifu wa hali ya juu. Wazingatie kanuni za mitihani  na taratibu, miongozo ya baraza waliyopewa ili kila mtahiniwa apate haki yake,” amesema.

Aidha, Dk. Mohamed ametoa wito kwa wakuu wa shule kutekeleza majukumu yao ya usimamizi kwa kuzingatia mwongozo wa usimamizi uliotolewa na NECTA na kuepuka kuingilia usimamizi wa watahiniwa ndani ya vyumba.

Kadhalika,  amesema baraza linawaasa wamiliki wa shule kutambua kuwa shule zao ni vituo maalum vya mitihani na hivyo hawatakiwi kwa namna yoyote kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani katika kipindi chote cha ufanyaji wa mitihani hiyo.

Amesema baraza halitasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na kusababisha udanganyifu kwa mujibu wa sheria.

Dk. Mohamed ameomba wadau kutoa taarifa katika vyombo husika kila wanapobaini  kuwapo kwa mtu au kikundi cha watu kinachojihusisha na udanganyifu wa aina yoyote katika kipindi chote cha mitihani na taarifa hizo ziwasilishwe baraza kupitia simu 0759 360 000 au kwa barua pepe [email protected].