Mao atoa somo, Stars ikirejea

By Saada Akida , Nipashe
Published at 09:29 AM Mar 28 2024
news
Picha: Taifa Stars.
Mastaa Simba, Yanga walioitwa Taifa Stars wakirejea nchini mapema

KIKOSI cha Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), kimerejea nchini jana alfajiri kikitokea Azerbaijan, ambapo ilishiriki mashindano maalum ya FIFA Series 2024, huku kiungo mkongwe, Himid Mao, akiwaasa wachezaji vijana kupambana na kulinda viwango vyao kwa sababu nchi inawategemea kuelekea katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), pamoja na AFCON ijayo.

Ikicheza kwenye Uwanja wa Dalga, Stars ilianza michuano hiyo kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Bulgaria na mchezo wa pili iliwachapa Mongolia mabao 3-0.

Akizungumza wakati wa kuwaaga wachezaji wenzake, Himid, aliwataka wachezaji vijana kuendelea kupambana  wanapokuwa katika timu zao ili kulinda viwango vyao kwa ajili ya kuisaidia Stars inayokabiliwa na michuano mbalimbali hivi karibuni.

"Wachezaji wenzangu napenda sana kuwashukuru wote, tunathamini sana mchango wa kila mmoja, kama unavyoona timu yetu imekuwa na vijana wadogo, wanahitaji sana uwepo wetu sisi wakongwe.

Tutaendelea kuwasapoti ili wafanye vizuri, sapoti yetu itawafanya waendelee kupambana hata wanapokwenda katika  klabu zao wajiamini, wafanye vizuri kwa sababu taifa linawahitaji sana kwenye michuano mbalimbali inayokuja,' alisema  mchezaji huyo wa zamani wa Azam FC  ambaye sasa anaichezea Tala'ea El Gaish SC ya Misri.

Taifa Stars itakuwa mwenyeji wa michuano ya CHAN itakayofanyika baadaye mwaka huu pamoja na AFCON ya 2027 ambayo itaandaliwa pamoja na nchi za Kenya na Uganda.