PPRA, ZPPDA zatia saini kuenzi Muungano

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:21 AM Apr 27 2024
Mkurugenzi Mkuu Mamlakaya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Eliakim Maswi na Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya Ununuzi na uondoaji wa Mali za Umma Zanzibar (ZPPDA), Othman Juma Othman wakisaini hati za makubaliano ya ushirikiano wa kiutendajiji.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mkuu Mamlakaya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Eliakim Maswi na Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya Ununuzi na uondoaji wa Mali za Umma Zanzibar (ZPPDA), Othman Juma Othman wakisaini hati za makubaliano ya ushirikiano wa kiutendajiji.

WAKATI Tanzania ikisherehekea miaka 60 ya Muungano, Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) na Mamlaka ya Ununuzi na Uondoaji wa Mali za Umma Zanzibar (ZPPDA) zimetia saini rasimu ya mkataba wa maelewano kufanya kazi pamoja na kuimarisha muungano.

Makubaliano hayo yalitiwa saini jana jijini Dodoma mbele ya wenyeviti wa bodi za wakurugenzi za mamlaka hizo, wawakilishi wa wafanyakazi na Makamu Mwenyekiti wa ZPPDA, wajumbe wa bodi zote mbili, Mkurugenzi Mkuu PPRA, Eliakim Maswi na Mkurugenzi Mtendaji ZPPDA, Othman Juma Othman na menejimenti ya PPRA.

Akizungumza baada ya kutia saini makubaliano hayo, Maswi alisema wamekubaliana kushirikiana katika kujenga uzoefu kwa watendaji na kukuza maarifa ya kiutendaji kwa kubadilishana utaalamu katika kutekeleza mbinu za kimkakati na taaluma ya ununuzi.

Pia  alisema watashirikiana katika kuzitambua sheria na miongozo ili kuleta tija na uwajibikaji ndani ya taasissi hizo, kuelimishana taarifa na ujuzi muhimu unaohusu ununuzi wa umma na uendeshaji mali za umma, kuhabarishana, kubadilishana uzoefu na kuhusishana katika fursa za kushiriki katika majukwaa na mikutano inayohusu ununuzi wa umma.

“Tumeamua kushirikiana kwa sababu wote tuko katika Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania na kazi tunazofanya zinafanana, hivyo  tumeamua kushirikiana na kubadilishana uzoefu katika utendaji kazi wetu hiyo ilikuwa ni mwaka 2022 na mwaka jana 2023 bodi yetu ya PPRA ilienda Zanzibar na kufanya kikao.

“Baada ya kikao kile viongozi wetu wa pande zote mbili walitoa maelekezo kwamba tukutane na tuandae makubaliano ambayo yatatuwezesha kushirikiana na kuwezesha pande zote mbili kufanya kazi,” alisema.

Maswi alisema wanasheria kutoka pende zote mbili wamefanya kazi kwa kushirikiana na wamewasilisha mapendekezo ambayo wameona yanafaa na PPRA imekubali kwamba yanafaa.

Aliongeza kuwa wamekubaliana kupeana msaada unaohitajika kupitia rasilimali walizonazo, kuwajengea uwezo watendaji wa pande zote mbili na kuwaweka pamoja.

“Baada ya mkataba huu mimi nikitaka mtu kutoka Zanzibar mwenzangu atamruhusu pia akitaka wa hapa kwetu nitamruhusu maana tunataka kubadilisha uzoefu, kutengeneza ushirikiano maalum katika shughuli za ufuatiliaji, ukaguzi na uchunguzi unaojumuisha uchunguzi wa uzingatiaji wa sheria na thamani ya fedha,” alisema Maswi.

“Pia tutashauriana kuhusu nyenzo za kisasa za utendaji wa majukumu ikiwemo vifaa vya kielektroniki na vingine vya kazi ya uchunguzi na ufuatiliaji. Tutakuwa na shughuli za pamoja ambazo tunazifanya ikiwemo kikao cha pamoja cha bodi ya Wakurugenzi, kila upande utakuwa na wajibu wa kuzingatia, kufuata na kutekeleza ratiba hiii,” alisema

“Ni wajibu wa pamoja kuandaa dira na ripoti itolewe ili kubuni mikakati ya kuleta tija katika nch yetu. Tumekubaliana kufanya mafunzo ya muda mfupi ya mara kwa mara kwa watendaji wetu wa mamlaka kwenda kwa kila mamlaka kujifunza yanayohusu shughuli za usimamizi wa mali za umma na uondoaji wa mali,” alisema.

Kupitia  makubaliano hayo, alisema wanaweza kufanya vikao vya pamoja vya dharura kama kuna changamoto imejitokeza ili kuimarisha Muungano na pia watakuwa wanawasiliana kupeana msaada unaohitajika kwa wakati muafaka kwa ajili ya kupeana mbinu za kutatua changamoto.

Naye Othman alisema: “Tunafanya kazi kwa pamoja kwa maslahi ya Watanzania. Tumetia saini makubaliano haya na yunaishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar imetoa maoni yake na leo hii yametuwezesha kufika hapa,” alisema.

Makamu Mwenyekiti Bodi ya ZPPDA, Ahmed Makame Haji, alisema makubaliano hayo yameishasainiwa lakini hayatakamilika kama hakutakuwa na utekelezaji wake.

 “Kama ambavyo tumekubaliana kuna umuhimu mkubwa wa kuhakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa na kujiwekea utaratibu wa kuangalia kama makubaliano hayo yanatekelezwa,” alisema.

Alisema kuna umuhimu mkubwa kufanya ufuatiliaji na kuangalia kila mwaka walipofikia katika utekelezaji wa makubalaino hayo na pale ambapo watabaini kasoro watazitatua na kuhakikisha wanafikia hayo makubaliano.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi PPRA, Dk. Leonada Mwagike, alisema baada ya kusaini mkataba kilichobaki ni utekelezaji kwa wakati ili kuhakikisha thamani halisi ya fedha inapatikana katika ununuzi wa umma .

Aliwataka kuhakikisha wanafanya tathimini ya utekelezaji wa makubaliano hayo mara kwa mara ili kuhakikisha mkataba huo unatekelezeka.