Samia ataja mambo matatu kuenzi Muungano

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 07:45 AM Apr 27 2024
news
Picha: Ikulu
Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Samia Suluhu Hassan akiwapungia mkono wananchi, alipowasili katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam jana, wakati wa sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

RAIS Samia Suluhu Hassan, ametaja mambo matatu makubwa katika kuenzi Muungano ikiwamo kutekeleza falsafa ya maridhiano, kustahimiliana, kuleta mageuzi na kujenga nchi, maarufu kama 4R.

Pia amewataka watanzania  kujivunia miaka 60 ya Muungano kwa kuwa  wamefanikiwa kuutunza na kuilinda nchi kwa kudumisha amani na utulivu.

Rais Samia aliyasema hayo jana katika sherehe za maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano zilizofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, zikibebwa na kaulimbiu isemayo: “Tumeshikamana, Tumeimarika kwa Maendeleo ya Taifa Letu.”

Sherehe hizo pia zilihudhuriwa na marais wa Kenya, Somalia , Burundi, Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia na Namibia. Pia ilihudhuriwa na Makamu wa Rais kutoka Malawi na Uganda, Waziri Mkuu wa Msumbiji, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda na mwakilishi wa marais kutoka Zimbabwe.

Akizungumza na Watanzania, Rais Samia alitaja mambo matatu makubwa, moja akiwataka watanzania kujivunia muungano huo.

“Ninataka kuwaambia Watanzania tuna kila sababu ya kujivunia Muungano wetu. Nchi ya Tanzania imetokana na maamuzi (uamuzi)  yetu (wetu) wenyewe.

“Katika kipindi chote cha miaka 60, taifa la Tanzania likiwa na watu na makabila 120 na linalounganishwa na lugha moja ya Kiswahili, wameimarisha Muungano na mshikamano.Tumeweza kuitunza na kuilinda nchi yetu kwa kudumisha amani na utulivu. Kupitia Muungano tumejenga umoja na mshikamano wa kitaifa.

“Tumeboresha udugu na bila shaka tumepiga hatua kubwa ya maendeleo kiuchumi, kisiasa na kijamii pamoja na kudumisha mila na desturi. Tuna kila sababu ya kujivunia Muungano”, alisema.

Jambo la pili, Rais Samia aliwasihi Watanzania katika kuuendeleza Muungano, kutekeleza falsafa ya maridhiano, kustahimiliana, kuleta mageuzi na kujenga nchi. Alisema hayo ndiyo yatakayoendelea kuwajengea amani na utulivu wa kudumu nchini na kuleta maendeleo endelevu.

“Leo hii tuna fahari kuwa nchi yetu imefika hadhi ya uchumi wa kati ngazi ya chini, na tathmini zote zinaonesha kuwa, kuna mwelekeo mzuri wa kuimarika na kufikia uchumi wa kati ngazi za juu, hivyo tuendelee kudumisha amani ya nchi yetu ili tujenge uchumi na kuleta ustawi zaidi wa wananchi,” alisema.

Rais Samia alitaja jambo lingine akiwataka Watanzania kuendelea kufanya kazi kwa bidii na maarifa zaidi ili wakuze tija na ustawi wa taifa, akikumbusha kauli isemayo ‘kazi ndicho kipimo cha utu’.

Alisema wanaposimama kutetea haki za Watanzania, hawana budi kutimiza wajibu ambao ni kufanya kazi kwa bidii ili kuwezesha haki za msingi zipatikane kwa maisha ya mwanadamu na kustawisha utu wa watu.

“Niwapongeze Watanzania kwa kutimiza miaka 60 ya Muungano hakika tumeshikamana na tumeimarika. Ninawashukuru wageni wetu kwa kuunga nasi katika maadhimisho haya, hii inamaanisha kwamba nchi yetu imejenga vyema uhusiano wa kidiplomasia,” alisema.

NDOTO CDF MWANAMKE

Katika sherehe hizo, Rais Samia alisema wameona tofauti ya Jeshi la Muungano na jeshi la tarabushi yalivyoonyesha maonyesho mbalimbali, huku akisifu kikosi cha bendera ambacho safari hii kina mwanamke.

“Na huu ndio mwanzo wa safari. Msije  mkashangaa mwaka 2030 tuna CDF (Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi) mwanamke hapa. Tulikuwa hatuwezi zile hustle (kupitia shida) za tarabushi lakini kwa maendeleo ya vikosi vya ulinzi sasa, tutakwenda bega kwa bega,” aliahidi.

MAUA KWA WAASISI

“Ninawashukuru kwa dhati waasisi Muungano huu, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume pamoja na viongozi waliofuata kwa kutuleta pamoja na kujenga taifa huru na madhubuti na lenye matumaini.

 “Zawadi pekee tunayoweza kuwapa ni kuendelea kudumisha muungano huu na kuenzi maono yao. Kwa msemo wa siku hizi tunasema, ‘tuwape maua yao’,” alisema.

Rais Samia alisema wamepata heshima na kuungwa mkono na wakuu wa nchi na serikali ya ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na viongozi waliowakilisha marais wao na pamoja na wadau wa maendeleo.

MVUA

Katika sherehe hizo, Rais Samia alimtambulisha mdau wa maendeleo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika ambaye yupo hapo kwa shughuli maalum na kumueleza kuwa, mvua imeharibu barabara na fedha zitatoka.

Rais Samia alisema anatambua wanaoathiriwa na mvua na kuwahakikisha kuwa serikali inafanya kila linalowezekana kurejesha miundombinu iliyoharibiwa.

Pia aliwataka wananchi kufuatilia taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) na kutoa pole kwa nchi jirani zilizokumbwa na maafa ya mvua hiyo.

Hata hivyo, Rais Samia alisema hali ya hewa ya mvua iliyonyesha jana haikuwezekana wote kuwapo uwanjani hapo, akiamini watanzania walikuwa wakifuatilia kupitia vyombo vya habari.

ILIVYOKUWA 

Miongoni mwa mambo yaliyofanyika uwanjani hapo na kuwa kivutio ni onyesho la kwata la askari wa zamani wajulikanao kama askari tarabushi kutoka Jeshi la Polisi ambalo wakati wote amri zikitolewa kutokana na changamoto ya lugha ya Kiingereza, walikosea.

Kwa mujibu wa Sajenti wa Polisi, Suleman Mwaimu, kikundi hicho kilipata umaarufu Zanzibar kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kuitwa askari wa tarabushi kwa kivazi cha kofia kinachoitwa tarabushi.

Amri zote katika gwaride hilo zinatolewa kwa lugha ya Kiingereza hali iliyosababisha askari kucheza kwa hofu na wasiwasi mkubwa na wakati mwingine kukosea kutokana na kutoelewa lugha.

Historia hiyo inakwenda tangu utawala wa sultan ambapo pamoja na kutawala Zanzibar mambo yote ya kiulinzi yalikuwa chini ya koloni la Uingereza.

Baada ya hapo kilifuata kikundi maalum cha Jeshi Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambalo lilionyesha kwata mbalimbali zinazotumika katika mapigano ya mjini ambapo helkopta maalum iliwasili kiwanjani hapo ikimshusha kiongozi wa kikundi maalum wa JWTZ akiwa angani kwa ajili ya kuelezea kwata mbalimbali zilizofanywa na jeshi hilo.

Sherehe hizo zilifanya licha ya idadi ndogo ya wananchi kujitokeza uwanjani hapo kutokana na mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia jana.