Uwanja wa Ndege Msalato kutumika Oktoba mwakani

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 11:07 AM May 08 2024
Uwanja wa Ndege Msalato kutumika Oktoba mwakani.
Picha: Maktaba
Uwanja wa Ndege Msalato kutumika Oktoba mwakani.

UWANJA wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato mkoani Dodoma ambao utakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege kubwa na abiria 1,500,000 kwa mwaka, unatarajiwa kuanza kutumika Oktoba mwakani.

Hayo yamesemwa na Msimamizi wa mradi huo Mhandisi wa Wakala wa Barabara nchini TANROADS, Mahona Luhende, wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini walipotembelea mradi huo.

Amesema mradi huo hadi kukamilika kwake utagharimu Sh. bilioni 360 ambazo ni mkopo nafuu wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) wakati serikali ya Tanzania ilitoa fidia kwa wananchi waliokuwa wanaishi eneo hilo.

Amesema uwanja huo unajengwa na kampuni mbili za Beijing Construction Engineering Group Co. Ltd inayojenga majengo ya uwanja huo na Kampuni ya Sinohydro Corporation Ltd inayojenga miundombinu ya barabara.

Amesema mkandarasi wa ujenzi wa majengo ya uwanja huo Beijing Construction alianza ujenzi huo Novemba mwaka 2022 na amefikia asilimia 22.5 na kwamba anatarajiwa kukamilisha ujenzi Oktoba mwaka 2025.

Amesema mkandarasi wa miundombinu ya barabara za uwanja huo amefikia asilimia 56 ya ujenzi.

“Mvua zilizonyesha zilisababisha baadhi ya shughuli kusimama na bila mvua huenda mkandarasi wa majengo ya uwanja angekuwa amefikisha asilimia 60 lakini tunafurahi kuona kwamba mkandarasi wa barabara za uwanja ameshafikia asilimia 56,” amesema.

Amesema sehemu ya kurukia na kutua ndege imefikia sehemu nzuri na kwamba wanatarajia mpaka Oktoba mwaka huu baadhi ya ndege zitaanza kupelekwa kutua kama sehemu ya majaribio.