Samia atoa maagizo mapya athari kimbunga Hidaya

By Elizabeth Zaya ,, Romana Mallya ,, Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:30 PM May 08 2024
Rais Samia Suluhu Hassan.
Picha: Maktaba
Rais Samia Suluhu Hassan.

WAKATI Rais Samia Suluhu Hassan akitoa maelekezo ya huduma za dharura kupelekwa maeneo yaliyoathiriwa na kimbunga Hidaya, hatua zimeanza kuchukuliwa ikiwamo kurejesha mawasiliano ya barabara ya Lindi-Mtwara na kuwapa misaada waathirika.

Maeneo hayo ni pamoja na Mafia mkoani Pwani, Kilwa mkoani Lindi na Ifakara mkoani Morogoro, ambayo yameathiriwa na kimbunga hicho baada ya kuripotiwa kuwapo nchini mwishoni mwa wiki iliyopita.

Katika kikao cha dharura cha Kamati ya Maafa Kitaifa ambacho Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alikiitisha juzi ili kupokea taarifa ya hatua zilizochukuliwa kwenye maeneo hayo, alisema Rais Samia ameelekeza huduma za dharura zipelekwe mara moja. 

Majaliwa alisema Rais Samia ameelekeza kuchukuliwa hatua za haraka katika maeneo yote yaliyoathiriwa na mvua zilizotokana na athari za kimbunga hicho ikiwa ni pamoja na kupeleka misaada. 

Aidha, alisema Rais ameagiza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lihakikishe linakamilisha uokoaji katika maeneo ya Kilwa na zaidi ya kaya 40 zimezingirwa na maji.

“Jeshi la Zimamoto mmefanya kazi kubwa, hakikisheni maeneo yenye makazi yaliyozingirwa na maji, wakazi wake wanaondolewa na kupelekwa maeneo salama pamoja na kupewa huduma zote muhimu,” aliagiza.

Majaliwa aliagiza Wizara za Ujenzi, Uchukuzi, Afya, Maji, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Mambo ya Ndani ya Nchi, Ulinzi na Fedha zichukue hatua za dharura ili kuhakikisha hakuna madhara zaidi yanayotokea katika maeneo yaliyopatwa na athari.

“Wizara ya Ujenzi endeleeni kuchukua hatua zote za dharura zinazohitajika kuhakikisha maeneo ya barabara yaliyokatika yanarekebishwa na huduma za usafiri zinarudi haraka,” aliagiza.

Alipongeza jitihada zinazofanywa na idara ya menejimenti ya maafa kwa kuendelea kufanya uratibu katika maeneo yote yaliyoathirika na kuwataka waendelee na uratibu katika maeneo yaliyopata madhara kuanzia juzi.

“Ongezeni nguvu katika maeneo ya Ifakara, Kilwa na Mafia na kuhakikisha wananchi wote walioathiriwa wanakuwa salama na wanapata huduma zote za msingi za kijamii,” aliagiza Majaliwa.

Waziri Mkuu pia, aliiagiza Kamati ya Maafa ya Kitaifa izisimamie kamati za mikoa na wilaya ili misaada inayotolewa kwa waathirika iwafikie walengwa.

BARARARA LINDI-MTWARA

Akizungumza wakati akiwa Nangurukuru wilayani Kilwa, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, alisema hadi kufikia leo au kesho barabara ya Lindi-Dar es Salaam itaanza kupitika, kutokana na serikali kutoa fedha za dharura kwa ajili ya kurejesha mawasiliano.

Mawasiliano ya barabara hiyo yalikatika tangu Jumapili na hivyo kusababisha abiria waliokuwa wakisafiri kuelekea mikoa ya Lindi, Mtwara na Dar es Salaam kukwama.

“Niendelee kuwatoa hofu wananchi na wasafiri wanaotumia barabara hii inayounganisha mikoa ya kusini, tangu jana (juzi) nimepiga kambi huku, nilianzia Somanga na sasa hivi tupo upande huu wa Nangurukuru, kama mnavyoona pande zote wanaendelea na kazi, bado tunaamini ndani ya saa 72, kufikia Alhamisi tutakuwa tumekamilisha kazi ya kurudisha mawasiliano ya barabara hii,” alisema Bashungwa.

Alimwagiza Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mohamed Besta, kuongeza idadi ya malori yanayosomba mawe pamoja na mitambo inayotumika kupakia mawe hayo katika magari, ili kuongeza kasi ya kujaza vifusi katika eneo la barabara yaliyosombwa na maji.

Bashungwa alisema kuwa pamoja na jitihada za kuagiza makalvati ya plastiki yanayotumika katika dharura za kurejesha mawasiliano ya barabara kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo kwa wakati, lakini watalazimika kutumia makontena kwa kuyakata yatumike kama mbadala wa kalavati na kuwezesha maji kupita.

"Tunahitaji mawe ya kutosha ya kujaza katika eneo la mita nne na la mita 100 na kuweka makaravati, niwahakikishie kwamba kazi hii tunaimaliza ndani ya saa 72 kama tulivyosema kwa kuwa kila kitu tumepata, vifaa tunavyo, mitambo ipo."

Eneo la barabara lililoharibika ni la mita 80 katika barabara ya Somanga-Mtama na pia tuta la barabara hiyo limekatika katika eneo la Mikereng'ende umbali wa kilomita 10 kutoka Somanga uelekeo wa Lindi.

Pia katika Lingaula barabara imekatika kwa umbali wa kilomita 12 kutokea Nangurukuru uelekeo wa Lindi.

Uharibifu wa barabara hiyo ulisababishwa na mvua kubwa zilizonyesha mwishoni mwa wiki mkoani humo zilizoambatana na upepo mkali.

WAATHIRIKA WAKUMBUKWA

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Kanda ya Kusini imekabidhi bati zaidi ya 100 zenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 2.7 kwa ajili ya waathirika wa mvua na upepo zaidi ya 300 kutoka vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Masasi ambao nyumba zao zimeezuliwa na kubomoka hivyo kukosa makazi ya kuishi hadi sasa.

Msaada huo umetolewa jana mjini Masasi na kukabidhiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa, Wilaya ya Masasi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Loutery Kanoni ili aweze kwenda kuwakabidhi waathirika hao.

Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo mwakilishi wa Taasisi ya TFS Wilaya ya Masasi, Mhifadhi Misitu Kanda ya Kusini, Anderson Besisila, alisema kutokana na wakazi zaidi ya 300 katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo kuathiriwa na mvua na upepo na kubomoa nyumba zao FTS kama wadau wameamua kutoa msaada huo wa bati zaidi ya 100 kwa ajili ya waathirika hao.

Besisila alieleza kwamba TFS imeguswa na jambo hilo na kuona kuna umuhimu wa kutoa msaada huo wa bati 100 zenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 2.7 ili kuhakikisha waathirika hao wanarejea katika mazao.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Loutery Kanoni, alisema kuwa anaishukuru TFS kwa kutoa msaada huo wa bati zaidi ya 100. 

Alisema katika Wilaya ya Masasi kuna zaidi ya waathirika 300 ambao wamepoteza makazi yao ya kuishi kwa kubomoka kufuatia mvua na upepo vilivyojitokeza wilayani hapa.

Kanoni alisema kuwa kufuatia athari hizo serikali wilayani Masasi iliomba msaada wa kuwasaidia waathirika hao ili kuweza kuwafariji na kwamba mwitio umekuwa chanya ambapo wadau mbalimbali wameshatoa misaada kama hiyo.

KIMBUNGA HIDAYA

Mei Mosi, mwaka huu TMA ilitahadharisha kuwapo kwa kimbunga hicho kutokea siku iliyofuata katika Bahari ya Hindi, kutokana na mkandamizo mdogo wa hewa Mashariki mwa Pwani ya Mkoa wa Mtwara.

Kwa mujibu wa TMA, mkandamizo huo mdogo wa hewa ulionekana kusogea kuelekea Pwani ya Tanzania na kuwapo kwake mpaka juzi (Mei 6).

Kutokana na kuwapo kwake, mvua kubwa iliyoambatana na upepo ilinyesha Mkoa wa Lindi na Mtwara na miongoni mwa athari ni pamoja zaidi ya madaraja manne wilayani Kilwa, barabara iendayo Dar es Salaam, yamesombwa.

Baadhi ya vijijini vimezungukwa na maji katika kata za Masoko, Mto Matandu, Songasi, Mitole, Likwatu, Mavuji na Machakama na zaidi ya watu 70 wako hatarini.

Athari nyingine ilijitokeza kwa vyombo vya usafiri baharini ambapo Jumamosi baadhi vilisimama kutoa huduma kwa siku moja baada ya kuwapo kwa upepo mkali.

Siku tatu zilizopita, mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa ilionyesha kuwa katika kipindi cha saa sita zilizopita, Kimbunga Hidaya kilipoteza kabisa nguvu yake baada ya kuingia nchi kavu katika kisiwa cha Mafia.

Mabaki ya mawingu ya mvua yaliyokuwa yakiambatana na kimbunga hicho yalisambaa katika maeneo mbalimbali ya ukanda wa Kusini mwa nchi hususan katika maeneo ya mikoa ya Lindi, Mtwara, Morogoro na maeneo jirani.