Bil. 11/- zalipwa kifuta machozi waathirika wanyamapori

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 02:03 PM May 08 2024
Naibu Waziri, Danstan Kitandula.
Picha: Maktaba
Naibu Waziri, Danstan Kitandula.

SERIKALI imesema kwa kipindi cha miaka saba Sh. bilioni 11.08 zimelipwa kama kifuta jasho na machozi kwa wananchi walioathirika na wanyama wakali na waharibifu.

Hata hivyo, Wizara ya Maliasili na Utalii ipo katika hatua za mwisho za majadiliano na Wizara ya Fedha ili kupata ridhaa ya matumizi ya viwango vipya vya fidia kwa kuwa viwango vilivyopo sasa vimepitwa na wakati.

Naibu Waziri, Danstan Kitandula, ametoa kauli hiyo jana bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Naghenjwa Kaboyoka.

Katika swali lake, Mbunge huyo aliyetaka kujua, katika kipindi hicho cha miaka mitano (2017 – 2022) ni kiasi gani cha fedha kimelipwa kama kifuta jasho kwa uharibifu wa mazao na watu kuuliwa na tembo.

Kitandula amesema kiasi hicho cha fedha ni kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018 hadi Machi, 2024.

Aidha, amesema tayari wizara imezifanyia marekebisho kanuni za kifuta jasho na machozi na kwasasa ipo katika hatua za mwisho za majadiliano na Wizara ya Fedha ili kupata ridhaa ya matumizi ya viwango vipya vya fidia kwa kuwa viwango vilivyopo sasa vimepitwa na wakati.

Amefafanua kuwa serikali imekuwa ikijitahidi kulipa fedha hizo kwa wakati inapopata taarifa kutoka kwenye halmashauri za wilaya na mchakato wa tathmini kufanyika ili kujua gharama halisi ya fedha inayotakiwa kulipwa.

Amesisitiza kuwa serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu kwa kujenga vituo vya askari kwenye makazi ya wananchi ili kuwasogeza karibu na maeneo yenye changamoto.

“Moja ya jitahada zilizofanywa na serikali ni kujenga vizimba vya kuzuia mamba wasidhuru wananchi wanapotumia maji ya mito au maziwa, pia kuandaa mfumo wa kielektroniki ili kuimarisha mfumo wa ukusanyaji na utunzaji wa taarifa za matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu,” amesema.

Pia amesema imeweka namba maalum za simu kwenye vituo vya kanda za kiutendaji za taasisi za uhifadhi kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kutoa taarifa za matukio ya wanyamapori bila malipo.