Wanging’ombe yapokea mabilioni ya elimu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:10 AM May 08 2024
Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Claudia Kitta.
Picha: Maktaba
Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Claudia Kitta.

HALMASHAURI ya Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe imepokea zaidi ya Sh. bilioni 1.03 kwa ajili ya elimu bila malipo kwa shule 120

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,  Agnetha Mpangile wakati akifungua kikao cha baraza la madiwani cha kipindi cha robo ya tatu kilichofanyika mjini hapa.

Mpangile, amesema halmashauri hiyo kupitia mapato ya ndani, imeendelea kuchangia ujenzi na ukalimishaji wa miundombinu ya elimu katika miradi ya maendeleo. 

Mwenyekiti huyo amewasisitiza madiwani na watendaji kuendelea kuwahamasisha wananchi kuchangia nguvu zao katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Nawasisitiza viongozi wa vijiji na kata kusoma mapato na matumizi kwa mujibu wa miongozo iliyopo ili kuweka uwazi wa mapato na matumizi ya fedha zote zilizopokelewa na kutumika kwenye shughuli za maendeleo, ikiwamo utambuzi wa nguvu za wananchi,” amesema Mpangile.

Awali Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Dk. Peter Nyanja, amesema kati ya halmashauri 184 nchini, Wanging’ombe ni kati ya halmashauri tano bora ambazo zinatumia mfumo wa Nesti.

Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Claudia Kitta, amewataka watendaji kusimamia miradi ambayo inatekelezwa kwa fedha zinatoka serikali kuu  ili iwe na  ubora kulingana na thamani halisi ya fedha.

Kitta amewakumbusha viongozi wilayani hapa kuhakikisha wanatatua kero za wananchi.

Diwani wa Kata ya Wanging’ombe, Geofrey Nyagawa, amesema miradi mingi ya serikali inayopelekwa katika maeneo yao haiwashirikishi wananchi. 

Wakati huo huo; Halmashauri ya  Wilaya ya Ludewa, imepokea zaidi ya shilingi bilioni 1 kwa ajili ya uchimbaji visima vya maji na kukamilisha miradi iliyokwama ili kuwezesha wananchi kupata maji ya uhakika na salama.

Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Jeremiah Maduhu, ameyasema hayo wakati wa kikao cha Jukwaa la Wadau wa Maji lililofanyika mjini hapa.

Maduhu, amesema serikali kupitia bajeti ya mwaka 2024/25 ilielekeza Sh. milioni 300 kutumika katika uchimbaji wa visima na Sh. millioni 700 kukamilisha baadhi ya miradi iliyokwama kabla ya Juni 30, mwaka huu.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Victoria Mwanziva, amewataka watendaji wa kata  na madiwani wa halmashauri hiyo kuunga mkono ajenda ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani kwa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maji katika maeneo yao na kuhakikisha inakamilika kwa wakati.

Mwanziva, amesema jukwaa hilo limeandaliwa madhubuti ili kujadili na kuhoji changamoto zilizopo katika miradi mbalimbali na kuzitatua ili kuwanusuru wananchi kutembea umbali mrefu kufuata  maji kwa matumizi ya kila siku.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Wise Mgina, amewasihi madiwani kuweka usimamizi mzuri ili kupata fedha hizo kwani vijiji zaidi ya 60 vinapata maji na vinakidhi baadhi ya vigezo.