PASADA yakumbuka waathirika mafuriko

By Joyce Lameck , Nipashe
Published at 06:18 AM Apr 27 2024
 Picha mbalimbali zikionesha zoezi la kukabidhi msaada kwa waathirika wa mafuriko Rufiji na Kibiti.
Picha: Mtandaoni
Picha mbalimbali zikionesha zoezi la kukabidhi msaada kwa waathirika wa mafuriko Rufiji na Kibiti.

SHIRIKA lisilo la kiserikali linalojihusisha na utoaji wa huduma kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI (PASADA), limetoa msaada wa vifaa vyenye thamani ya Sh. milioni nane kuwasaidia waathirika wa mafuriko katika wilaya za Rufiji na Kibiti.

Shirika hilo lililo chini ya Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, lilitoa msaada huo juzi jijini Dar es Salaam ambao baadaye ulipelekwa kwenye maeneo hayo kwa ajili ya kugawa kwa waathirika.

Misada iliyotolewa na PASADA ni pamoja na  magodoro na ndoo zenye koki kwa ajili ya kuwasaidia waathirika hao kuishi katika mazingira safi ili  kujiepusha na magonjwa yatokanayo na mafuriko.

Akizungumnza wakati wa ibada maalumu ya kuviombea vifaa hivyo, Askofu Msaidizi Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Henry Mchamungu, alitoa wito kwa mashirika mengine nchini kujitokeza kuunga mkono juhudi za kuwasaidia waathirika.

Askofu Mchamungu alilishukuru shirika hilo kwa kuguswa na kutoa mchango wa vitu ambavyo vitawasaidia kutokana na athari zilizowakumba wakazi wa maeneo hayo.

“Ninawashukuru PASADA kwa moyo wao wa kujitoleo magodoro pamoja na ndoo zenye koki ambazo zitasaidia katika usafi, kama tunavyojua kuwa mafuriko huwa yanaambatana na magojwa ya mlipuko.

“Pamoja na PASADA kutoa msaada huo, Jimbo Kuu la Dar es Salaam  bado linajipanga kwa ajili ya kutoa msaada kwa wale walioathirika na mafuriko katika maeneo hayo,” alisema Mchamungu

Mkurungezi wa Huduma na Tiba wa PASADA, Eugene Filbert, alisema lengo la kutoa vifaa hivyo ni kuzisaidia familia zilizokumbwa na mafuriko.

Pia alitoa wito kwa viongozi wa maeneo hayo kuhakisha vifaa hivyo vinawafikia walengwa walioathiriwa ili kuwasaidia katika kipindi hiki kigumu wanachopitia.

Mkurungezi Mtendaji wa Pasada, Cayus Mrina, alisema lengo la kutoa msaada huo ni kuunga mkono juhudi za serikali katika kupambana na maafa.