Bil. 19/- zahitajika kukarabati miundombinu

By Christina Haule , Nipashe
Published at 09:28 AM May 08 2024
Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Ndyamukama.
Picha: TAMISEMI-Morogoro
Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Ndyamukama.

SHILINGI bilioni 19 zinahitajika kurejesha hali stahimilivu ya miundombonu ya barabara za mijini na vijijini iliyoharibiwa na mvua za El-nino kwenye wilaya mbalimbali mkoani hapa.

Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Ndyamukama, alisema hayo jana wakati akiongea na waandishi wa habari kuwa katika uharibifu wa mwanzo serikali ilitoa Sh. bilioni 2.8 ambazo utekelezaji wake ulikwama kutokana na mvua kuwa kubwa.

Mhandisi Ndyamukama alisema utekelezaji wa ukarabati wa miundombinu ya barabara hizo utaanza baada ya hali kukaa sawa ndani ya mwezi Mei kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA).

Alisema mvua inayoendelea kunyesha imeharibu sehemu kubwa ya miundombinu kwenye mkoa hasa katika wilaya za Ulanga, Kilombero, Malinyi na Mlimba na kuvuruga utaratibu wa kawaida wa matengenezo ya barabara waliojiwekea.

Aidha, Mhandisi Ndyamukama alisema katika mwaka wa fedha 2023/24 mkoa ulipokea bajeti ya barabara ya Sh. bilioni 26 kwa ajili ya kutekeleza maboresho ya barabara fedha zilizotoka Serikalini kupitia fedha za mfuko wa barabara, mfuko wa jimbo na mfuko wa tozo.

Alisema wakati wakiwa karibu asilimia 50 ya utekelezaji wa mpango wa kawaida wa maboresho ya barabara ndipo mkoa ukakumbwa na changamoto ya El-nino na kusababisha utekelezaji wa bajeti husika kusimama.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga mkoani hapa, Edson Wiliamsoli, aliiomba TARURA na TANROADS kuongeza juhudi za kukarabati miundombinu hiyo ili kurejesha mawasiliano katika maeneo mbalimbali ikiwamo daraja la eneo la Ketaketa ambalo awali lilijengwa na TARURA na kugharimu Sh. milioni 700, lakini kwa sasa limekatika.

Aliyataja madaraja mengine yaliyokatika kuwa ni ya kwenye maeneo ya Ngongo, Mwaya na Libenanga na nguvu za wananchi akiwamo mbunge wa jimbo hilo Hasham Alaudin kuweka mawe kwenye baadhi ya maeneo zilisaidia baadhi ya maeneo kupitika kiasi.