Watanzania watakiwa kuchangamkia biashara hewa ukaa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:22 AM May 08 2024
Hewa ya ukaa.
Picha: Mtandaoni.
Hewa ya ukaa.

WATANZANIA wametakiwa kuchangamkia fursa za biashara ya hewa ya ukaa kutokana na kuwa na faida nyingi ikiwamo kupata fedha nyingi.

Rai hiyo imetolewa jana na Meneja Mpango wa CookFund wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF), Emmanuel Muro, wakati wa mjadala uliohusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, biashara ya hewa ukaa.

Muro alisema: “Ni fursa kwa Watanzania kuanza kushiriki katika biashara ya hewa ya ukaa.  Biashara hii siyo kwamba unaanza leo na kuvuna kesho, ni lazima uwe na subira na uvumilivu, misitu tunayo, uzalishaji wa hewa upo, wanunuzi wapo nje ya nchi. Ni suala la kujua nani nimfuate, nani nimshirikishe”.

Alisema UNCDF kupitia mpango wa nishati safi ya kupikia linaunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan wa matumizi ya nishati safi.

Alisema Tanzania ina takribani hekta milioni 48.1 za rasilimali za misitu, sawa na asilimia 55 ya ardhi yote ya Tanzania Bara ambayo ikitumika vizuri kupitia miradi ya biashara ya kaboni ni suluhisho muhimu la kupunguza kasi ya uharibifu na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa. 

Alisema fursa hiyo kubwa pamoja na fursa nyingine kama vile ardhi oevu vinaweza kutoa faida zaidi katika ufadhili wa kaboni kwa wawekezaji wa ndani.

Mhifadhi wa uoto wa asili kutoka NCMC, Dk. Paul Lyimo, alisema jamii kubwa ya Watanzania inatumia kuni na mkaa katika kupikia.

Alisema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012, kaya milioni 13.9 Tanzania wanatumia kuni na mkaa katika kupikia.

Alisema: “Tanzania kuna fursa zaidi ya matumizi ya hewa ya ukaa kwa sababu nusu ya nchi imejaa misitu. Tunapaswa kujielekeza katika biashara ya hewa ya ukaa”.