SERIKALI kupitia Kamati ya Maboresho ya Mfumo wa Kodi, inaendelea kufanya uchambuzi na tathmini ya mifumo ya kodi, ada na tozo za huduma kwa lengo la kuondoa urasimu na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande, alisema hayo juzi bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Fakharia Shomar Khamis.
Katika swali lake, mbunge huyo alihoji kwa nini kodi ya jengo na kodi ya ardhi zisiunganishwe na kuwa moja ili kumwondolea usumbufu mwananchi.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Chande alisema tathmini hiyo inajumuisha mapendekezo ya maboresho ya mfumo wa usimamizi wa kodi ya jengo na kodi ya ardhi kama inavyopendekezwa na mbunge huyo.
Sambamba na hatua hiyo, alisema serikali inaandaa mfumo wa kielektroniki wa kutoa ankara ya pamoja kwa huduma zinazolandana ili kuondoa usumbufu kwa wananchi wanaostahili kulipa kodi ya jengo na kodi ya ardhi.
Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Mwera (CCM), Zahor Mohamed Haji, alisema kwa kuwa suala la utafiti linahitaji muda, hivyo serikali iwaambie wananchi lini itakamilisha kazi hiyo.
“Mifumo ni jambo kubwa na je, serikali iko tayari kuendelea kutoa elimu zaidi kwa wadau?”alihoji.
Akijibu swali hilo, Chande alisema tathmini hiyo ni sehemu ya maandalizi ya muswada wa sheria ya fedha ya mwaka 2024 ambao utawasilishwa bungeni katika mkutano huu wa bunge.
Alisema serikali kupitia taasisi zake zimekuwa zikitoa mafunzo kwa wadau siku kwa siku kulingana na mahitaji.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED