Samia akiwa mwalikwa Jumatatu, fahamu maudhui ya kikao cha G20 na historia yake

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:26 AM Nov 15 2024
Ndivyo ilivyokuwa kikao cha G20 nchini India, mwaka jana.
Picha: Mtandao
Ndivyo ilivyokuwa kikao cha G20 nchini India, mwaka jana.

AKIWA na miezi kadhaa tangu kuingia madarakani, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akahutubia Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kwenye makao makuu yake jijini New York, Marekani, ikiwa ni mara ya kwanza tangu ashike wadhifa huo mwezi Machi.

Hapo akawa anamulika masuala mbalimbali kuanzia uchumi, siasa, tabianchi, usawa wa jinsia na janga la Covid – 19 lililokuwa linapamba moto wakati huo.

Rais Samia katika hotuba yake ya kwanza ana kwa ana kwenye mjadala huo, ambayo kiuchumi na kidiplomasia ikafafanuliwa kuwa na maana kubwa na muhimu kwake.

Hapo akaanza na dhana ya ushirikiano wa kimataifa, akitamka katika ujumbe uliotoa mvuto kwa kutamka:“Chini ya uongozi wangu, Tanzania itaendelea kuwa mshirika muhimu wa Umoja wa Mataifa na muungaji mkono wa kutegemewa wa suala la ushirikiano wa kimataifa.

“Tutanyoosha mkono kwa wale wanaotukumbatia na kushirikiana nasi. Tutaendelea kuwa Tanzania ambayo mmeifahamu kwa muda mrefu.

“Tanzania yenye amani na ambayo inashirikiana na chi zote kubwa au ndogo, zenye nguvu au zisizo na nguvu, tajiri au masikini kuifanya dunia dunia yetu kuwa bora kwa ajili yetu sote.”

Ushuhuda na mwendelezo wa ahadi ya kwanza na mwendelezo wa utekelezaji wa mialiko, sasa anapata mialiko mingi kimataifa, inayombebesha heshima kimataifa duniani, Jumatau ijayo akitarajiwa kuwapo jijini Rio De Janeiro Brazil, kwa siku mbili.

Huo ni mkutano wa viongozi wa kundi la nchi 20 zinazohimili uchumi wa dunia, mwaliko ukitolewa na Mwenyekiti wao, Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil, huku Dk. Samia akiweka rekodi kuwa Rais wa kwanza mwanamke kuhudhuria mkutano wa viongozi wa kundi hilo, tangu kuitwa G20 mwaka 2009, ikipanda kutoka kundi la nchi nane, G8.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, inaonesha kuwa marais wastaafu  nchini Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete, walishiriki mikutano ya G8 iliyofanyika mwaka 2005 na 2008.

Kimsingi, kundi la G20 linaundwa na mataifa ya: Argentina, Australia, Brazil, Canada, China, France, Ujerumani, India, Indonesia, Italy, Japan, Jamhuri ya Korea, Mexico, Russia, Saudi Arabia, Afrika Kusini, Uturuki, Uingereza na Marekani. 

Pia, kuna wanachama wa kitaasisi; Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Ulaya (EU), ambao mara nyingi unawakilishwa na rais wake. 

Vilevile kuna wadau; taasisi zinazowakilishwa na watedaji wake wakuu, ambazo ni: Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF); Benki ya Dunia (WB); pia Kamati ya Maendeleo ya IMF na Benki ya Dunia

Aidha, kimuundo G 20 hufanya kazi bila ya sekretarieti ya kudumu wala wafanyakazi na uenyekiti wake huzunguka kila mwaka, kati ya wanachama na mwenyekiti anatokana na mmoja wa mataifa waasisi.

Mwenyekiti  aliyeko, huunda sekretarieti ya muda kwa wakati wake, inayoratibu kazi ya kikundi na inapanga mikutano yake. 

Safu hiyo ya uenyekiti tangu chombo hicho kianze, iko ifuatavyo kihistoria ya nchi na msaka husika katika mabano: 2001 ni Ujerumani na kisha Canada mwaka huo; ikiafuata India (2002), Mexico ( 2003), Ujerumani (2004),China (2005), Australia (2006), Ufaransa (2007), Marekani (2008) na  Uingereza (2009),

 | Wengine ni: Korea Kusini (2010), Ufaransa (2011), Mexico (2012), Russia (2013), Russia (2014), Uturuki (2015), China (2016), Ujerumani (2017), Argentina (2018), Japan (2019), Saudi Arabia (2020), Italia (2021), Indonesia (2022)  na India mwaka jana.  

Pia, Umoja wa Afrika (AU) umejumuishwa kuwa mwanachama wa kudumu katika muungano G20 katika mkutano uliokamilika nchini India mwaka jana na sasa una hadhi sawa na Umoja wa Ulaya (EU). 

Viongozi wa mataifa wanachama wa G-20 hukutana kila mwaka mara mbili katika Kongamano la G-20.  

G-20 hufanya kazi bila sekretarieti ya kudumu wala wafanyakazi. Uenyekiti huzunguka kila mwaka kati ya wanachama na huchaguliwa kutoka kwa kambi tofauti za nchi. 

MIKUTANO G20

Historia ya Makongamano ya G-20, yalianzishwa ikiwa mwitikio wa tatizo la fedha kati ya mwaka 2007 hadi 2010, pia kuonekana nchi zinazostawi hazikujumuishwa vya kutosha katika majadiliano ya kiuchumi duniani na utawala. 

 Makongamano ya G-20 ya wakuu wa nchi au serikali yalifanyika mbali na mikutano ya G-20 ya mawaziri wa fedha na magavana wa benki kuu, walioendelea kukutana kuandaa kongamano la wakuu wa nchi, pia kutekeleza maamuzi yao. 

SAFARI ZA SAMIA

Pata historia ya ziara ambazo amefanya Rais tangu kuingia madarakani miaka mitatu na nusu sasa.         

Mwaka 2021; Rais  Dk. Samia akianzia mwezi Aprili alifanya ziara za kujenga uhusiano katika nchi jirani na hata kushuhudia uchaguzi katika Afrika Mashariki,  Uganda, Kenya, Burundi na huko Msumbuiji katika kikao cha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). 

Katika historia hizo, baadhi ya maeneo kama Burundi akifika zaidi ya mara moja na baada ya nusu mwaka kuanzia mwezi Julai, pia akafika nchi za Malawi, Rwanda na Zambia alikohudhuria matukio muhimu.

 Baadaye kuanzia mwezi Septemba ya mwaka huo 2021, Rais Dk Samia akafika katika mataifa ya Marekani, Uingereza, Misri na Scotland katika safu yake ya umahiri, kikao cha hali ya hewa duniani. 

 MWAKA 2022

Ni mwaka huo akazuru nchi zaidi ya 15 akiwajibikia nchi kiuchumi na diplomasia ya uhusiano mwema, huku akiwa na mvuto uliompatia mialiko mingi kimataifa.

Hapo kunatajwa mataifa kama Msumbiji,  Ufaransa, Ubelgiji kwenye kikao cha pamoja cha AU na EU; pia akafika Jamhuri ya Emerati (UAE) kwenda kuimarisha biashara ya nchi, Marekani akaenda kuzindua Sinema ya Royal Tour katika  majiji ya Washington, New York na Los Angeles, mchakato uliochukua  zaidi ya wiki, sasa ‘ikijibu’ katika biashara ya utalii kimataifa.

Baadae akawa katika ziara za uhusiano kati ya mwezi Mei na Julai huko Kampala, Uganda; Accra Ghana, Muscat, Oman; na Dakar Senegal. 

Kuanzia mwezi Agosti akajumuika na wakuu wa nchi za SADC huko Kinshasa, DRC, pia akawapo katika uchaguzi mkuu wa nchini Kenya mwezi uliofuata na maziko ya Malkia Elizabeth II wa Uingereza, ikizingatiwa Tanzania ni  tabaka la Jumuiya ya Madola.  Safari ya Rais Dk. Samia mwezi huo ikamfikisha Msumbiji, safari hiyo akiwa makao makuu Maputo na ziara ya 2021, alikuwa Pemba kunakoathiriwa na hali ya hewa.

 Oktoba akawa Doha, Quatar kwa kikao mahsusi kuhusu afya ya umma na dunia, kisha mwezi Novemba akaendeleza uhusiano na ndugu wa taifa walioko Beijing, China na kurejea kikao cha hali ya hewa (COP) wenye hali ya hewa kama kinachoendelea hivi sasa kwa mwaka huu, hadi tarehe 22. Kufika mwezi Desemba, Rais Dk. Samia alikuwa Marekani katika mkutano wa viongozi duniani.

 MWAKA 2023 

Mapema mwaka jana. Rais alikuwa Davos Uswisi, kujadili uchumi wa dunia, kisha akarejea kikaoni kwa Waafrika wenzake huko, Dakar Senegal  anakokanyaga kwa mara ya pili. Baadaye, Februari Rais akawapo katika kikao cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Bujumbura, Burundi na mwezi huo akawapo Addis Ababa, Ethiopia kwa kikao cha AU.

 Pia, akawa na ziara za Afrika Kusini, Windhoek, Namibia, Uganda, Nigeria kwenye uchaguzi, akakanyaga tena nchini Malawi kwenye uchaguzi, Mnamo Agosti akawa Johannesburg, Afrika Kusini, ilipofika Septemba akahudhuria kikao cha hali ya hewa mwezi huo akijadili hali ya hewa. 

Pia, kukawapo kilimo cha kisasa huko Doha, Quatar na akaendeleza uhusiano ziarani India mwezi huo wa Oktoba, hali kadhalika Zambia. Dk. Samia kaendeleza ziara hizo, akihudhuria kikao cha utalii duniani nchini Rwanda na akarejea kikao cha wakuu wa nchi wa SADC huko Luanda, Angola,  kikao cha uwekezaji wa Benki ya Afrika huko Morocco na Mkutano wa Afrika, Saudi Arabia. 

Kisha akarejea huko huko urabuni UAE, kuhudhuria kikao cha hali ya hewa, kilichoanza mwishoni mwa Novemba na kumalizika Desemba.

MWAKA 2024 

Taarifa za safari za rais mwezi huu zinagusa; nchi za Indonesia kudumisha uhusiano, makao makuu ya katoliki Vatican City, pia Norway; kwenye kikao cha AU huko Addis Ababa, Ethiopia; Windhoek, Namibia, Uturuki, Kenya (mkutanoni) na Ufaransa. 

Pia, kuna ziara tofauti za Afrika Kusini na Rwanda, kwenye matukio ya uchaguzi; vikao vya SADC huko Zimbabwe na AU nchini Kenya katika mwezi huo wa Agosti; mwezi Septemba akahudhuria kikao cha uhusiano wa Afrika na China, kilichofanyika huko Beijng China na hivi karibuni alikuwa na kikao kingine Marekani.