DC awasihi Watanzania kulinda, kuenzi Muungano

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 07:08 AM Apr 27 2024
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Joseph Mkude.
Picha: Marco Maduhu
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Joseph Mkude.

MKUU wa Wilaya ya Kishapu, Joseph Mkude, amewasihi Watanzania kuendelea kuuenzi na kuulinda Muungano kwa vizazi vyote ili kuendelea kufurahia amani, umoja na mshikamano.

Waasisi wa Muungano, Hayati Abeid Amani Karume, ambaye alikuwa Rais wa kwanza Zanzibar na Hayati Julius Nyerere, Rais wa kwanza Tanganyika, waliunganisha Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, 1964  na kuwa Tanzania.

Mkude alisema hayo juzi kwenye mkesha wa kusherehekea miaka 60 ya Muungano wilayani hapa. 

Alisema Watanzania wanaposherehekea miaka 60 ya Muungano, hawana budi kuwaenzi waasisi hao kwa kuendelea kudumisha amani,mshikamano,upendo na umoja ili nchi iendelee kuwa tulivu na kusongambele kimaendeleo.

Pia alisema kupitia Muungano huo, hali ya ulinzi na usalama inaendelea kuimarika kwa pande zote na amani kuendelea kutawala, huku akiwapongeza marais wote hadi wa sasa, Dk. Samia Suluhu Hassan na Dk. Husein Mwinyi kwa kuendelea kuuenzi na kuulinda Muungano.

Kaulimbiu katika Sherehe za miaka 60 ya Muungano inasema: "Miaka 60 ya Muungano wa Tanzania, Tumeshikamana, Tumeimarika kwa Maendeleo ya Taifa Letu".