Rais Samia atoa msamaha kwa wafungwa 1,082

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 09:35 PM Apr 26 2024
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni.
Picha: Maktaba
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni.

RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa msamaha kwa wafungwa 1,082 ambapo 29 kati yao wameachiwa huru leo na wengine 20 waliokuwa wakitumikia adhabu ya kifo wakibadilishiwa kuwa kifungo cha maisha.

Kwa mujibu waa taarifa yake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni , wafungwa hao wamepata msamaha huo ikiwa ni maadhimisho ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika taarifa hiyo iliyotiwa saini na  Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Daniel Sillo, kwa niaba ya Waziri, inasema wafungwa 27 waliohukumiwa kifungo cha maisha wamebadilishiwa adhabu na kuwa kifungo cha miaka 30.

Pia, wafungwa 1,006 wamepunguziwa adhabu zao na watabaki gerezani na kuendelea kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.

"Ni matarajio yetu serikali kuwa wafungwa walioachiliwa huru leo Aprili 26, watarejea tena katika jamii kushirikiana na wananchi katika ujenzi wa taifa na kwamba watajiepusha na makosa ili wasirejee tena gerezani," inasema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo inasema wafungwa wote wenye sifa stahiki wapunguziwe robo ya adhabu zao wanaozitumikia hivi sasa baada ya kutoa punguzo la kawaida la moja ya tatu linalotolewa chini ya kifungu cha 49 (1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58.

Inasema wafungwa hao sharti wawe wamehukumiwa robo ya adhabu zao gerezani na wawe wameingia gerezani kabla ya Desemba 28, 2023, isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika sharti la 2(i-xi).

Kadhaliaka, wafungwa wagonjwa wenye magonjwa ya kudumu au sugu ambao wapo kwenye hatua ya mwisho, ugonjwa na hatua hiyo vidhibitishwe na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

“Wafungwa wa kike walioingia na ujauzito gerezani au wenye watoto wanaonyonyesha au wasionyonya. Wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili wasio na uwezo wa kufanya kazi.

“Ulemavu huo uthibitishwe na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu/ Mganga wa Wilaya. Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kuwekwa kizuizini ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka 10 au zaidi.

Baadhi ya makosa ambayo hayahusiani na msamaha huo taarifa hiyo inasema ni wafungwa wanaotumikia vifungo vya nje na wale waliowahi kukiuka masharti ya vifungo vya nje ya Sheria ya Bodi ya Parole Sura ya 400 (R.E 2002), Sheria ya Huduma kwa Jamii Sura ya 291 (R.E 2002 na kanuni ya kifungo cha nje.

Pia wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifugo gerezani ambacho siyo cha maisha kwa makosa ya uhujumu uchumi, matumizi mabaya ya madaraka, utakatishaji fedha, rushwa na usafirishaji au kujihusisha kwa namna yoyote ile na dawa za kulevya ikiwamo bangi.

“Wanaotumikia kifungo gerezani ambacho siyo cha maisha kwa makosa ya wizi au ubadhirifu wa fedha za serikali. Makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali au kutendeka kwa makosa hayo.

Pia hauwahusu wenye makosa ya waliojaribu kuua, kujaribu kujiua au kuua watoto wachanga, ugaidi, uharamia na makosa ya kimtandao.