Watumishi wazembe, wabadhirifu waonywa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:40 AM May 07 2024
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evance Mtambi.
PICHA: MAKTABA
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evance Mtambi.

MKUU wa Mkoa wa Mara, Kanali Evance Mtambi, amewaonya watumishi wa umma wazembe kazini wakati wa kutoa huduma kwa wananchi.

Aidha, amewaonya kutohujumu fedha za miradi ya maendeleo na kuwataka kufanya kazi kwa uadilifu na kuepuka vitendo vya rushwa.

Ameyasema hayo wakati wa ziara yake wilayani Tarime, soko jipya linalojengwa akiongozana na Mkuu wa wilaya hiyo, Kanali Maulid Surumbu, wenyeviti wa halmashauri za Tarime mji, Daniel Komote, Saimon Kles wa Tarime Vijijini na wakurugenzi wa halmashauri hizo, Gwimbana Ntovya na Solomon Shati kamati za ulinzi mkoa na Wilaya Tarime.

Kanali Mtambi amesema atawashughulikia watumishi wazembe kazini, wala rushwa, wanaohujumu fedha za miradi ya maendeleo inayoletwa na serikali ikiwamo ya ujenzi wa vituo vya afya, zahanati, madarasa, barabara, maji na watakaobainika kujihusisha na vitendo vya ubadhirifu wa mali ya umma atawakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

"Soko hili la Tarime limechukua muda kukamilika mnadai kuna changamoto zilikuwapo za upatikanaji wa kokoto mara mvua na malipo kwa mkandarasi zaidi ya bilioni moja serikali ilishatoa fedha za mradi huu wa kukamilisha soko hili na kwa mkandarasi ahakikishe majengo ya soko hili linajengwa kwa viwango vilivyotakiwa na vipimo sahihi bila kuhujumiwa.

"Huko Tarime Vijijini nimepita Kata ya Mriba, Tarafa ya Ingwe ninaambiwa kuna utoro wanafunzi zaidi ya 40 wa kike wameshindwa kuhudhuria masomo bila sababu na baadhi yao huenda wametoroshwa, wazazi, walimu na uongozi wa kata na tarafa wanatakiwa kufuatilia utoro huo ili wahusika waliowatorosha wanafunzi hao kuchukuliwa hatua za kisheria,'' amesema Mtambi.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tarime Mji, Gwimbana Ntovya, amesema kuwa 'Soko jipya la Tarime ujenzi umefikia asilimia 87 bado ukamilishaji wa milango na sehemu ya mbele yenye vibanda 325 vya maduka, vidimba 160, bucha tatu, migahawa miwili, super market moja, benki mbili na kukamilika kwa soko hilo kutasaidia kukusanya mapato ya zaidi ya Sh. milioni 588 kwa mwezi fedha ambazo zitasaidia katika ujenzi wa miradi ya umma katika halmashauri.